HOTUBA YA MAKAMU WA RAIS
Ndugu Wajumbe, naomba nianze kwa kufuata mfano wa wenzangu walionitangulia, kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kukutana hapa tukiwa na afya njema katika siku hii muhimu kwa mustakabali wa Muungano wetu. Ningependa pia kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kunikabidhi kijiti hiki cha kusimamia masuala ya Muungano, akiwa ameacha msingi mzuri wa kuendelea kutafutia ufumbuzi changamoto za Muungano.
Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati wajumbe wote wa kikao hiki kwa kazi kubwa na ushiriki wenu mzuri katika vikao vya wataalam kuhakikisha changamoto zinazoukabili Muungano wetu zinatafutiwa ufumbuzi. Nafahamu haikuwa rahisi kufanya hivyo, ila kwa kuwa mna ari na nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa Muungano wetu adhimu na adimu unadumishwa na kustawi kwa kila hali, ndio maana leo hii tumeweza kutatua changamoto kumi na moja (11) ndani ya kipindi cha miaka miwili, ambapo hoja tisa (9) zimeandaliwa hati za makubaliano na kusainiwa leo na hoja mbili (2) ni za kiutendaji ambazo hazihitaji kuandaliwa hati. Nawapongeza sana.
Ndugu Wajumbe, hafla hii ni muhimu sana kwani ni uthibitisho thabiti kuwa, Kamati hii inafanya kazi kubwa sana katika kulinda na kuimarisha Muungano wetu kwa kuhakikisha kwamba, wananchi wa pande zote mbili za Muungano wananufaika na matunda ya Muungano wetu.
Hii pia inatoa fursa kwa wananchi kuwa na uelewa mpana kuhusu jitihada mbalimbali ambazo zinachukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutatua changamoto za Muungano.
Ndugu Wajumbe, tukio hili linafanyika kwa mara ya tatu, mara ya kwanza lilifanyika hapa Zanzibar tarehe 2 Juni, 2010 Salama Hall, Bwawani na mara ya pili tarehe 17 Oktoba, 2020 katika Ikulu ya Dar es Salaam. Nina imani utaratibu huu ulio ndani ya mwongozo wetu utaongeza ari na hamasa kwa pande mbili za Muungano kuzidisha ushirikiano na hatimaye kuulinda na kuudumisha Muungano wetu. Makubaliano yaliyofikiwa leo yatakuwa na faida zifuatazo kwa pande zote za Muungano:-
Moja, kutungwa kwa Sheria ya Kusimamia na Kuendeleza Uvuvi wa Bahari Kuu, Sheria Na. 5 ya mwaka 2020 kutaongeza ufanisi katika usimamizi na uendelezaji wa uvuvi wa Bahari Kuu na kuhamasisha uwekezaji katika uvuvi wa Bahari Kuu.
Pili, makubaliano juu ya usimamizi na mgawanyo wa ajira katika Taasisi za Muungano yataongeza hamasa na manufaa kwa wananchi wa pande mbili za Muungano kutumia fursa zilizopo katika Muungano wetu;
Tatu, makubaliano juu ya utaratibu wa mgawanyo wa mapato yatokanayo na misaada ya kibajeti kutoka nje (GBS) na misaada ya kibajeti ya kisekta yataongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo;
Nne, kusainiwa kwa Mkataba wa Mkopo wa Fedha za Mradi wa Ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja kutaimarisha huduma za afya kwa wananchi wetu;
Tano, kusainiwa kwa Mkataba wa Mkopo wa Ujenzi wa Barabara ya Chake Chake hadi Wete – Pembakutaimarisha huduma za kijamii kwa kurahisisha mawasiliano na kuharakisha maendeleo ya nchi;
Sita, kupitiwa kwa gharama za ujenzi wa mradi wa Bandari ya Mpigaduri na kubaini kuwa gharama hizo ni kubwa sana, hivyo, SMZ kufanya uamuzi wa kuvunja mkataba na CHEC ni jambo la busara sana ambalo limeepusha nchi kuingia kwenye hasara;
Saba, kufanya maboresho ya Mfumo wa ukokotoaji na ukusanyaji wa kodi kwenye huduma za simu kumeondoa malalamiko kutoka kwa Makampuni ya simu na kunaimarisha mazingira ya uwekezaji;
Nane, ni jambo la busara sana kuruhusu mapato yanayotokana na Tozo za VISA kutumika pale yalipokusanywa kama ilivyo kwenye mapato mengine ya Muungano; na
Tisa, Makubaliano ya uingizaji wa maziwa ya AZAM katika soko la Tanzania Bara yanaondoa malalamiko ya mwekezaji lakini pia kuendelea kuimarisha biashara na ajira nchini.
Ndugu Wajumbe, Nia na Madhumuni ya haya yote ni kuuenzi, kuulinda na kuudumisha Muungano wetu. Napenda nitumie fursa hii kutoa rai kwa taasisi zote husika kuwa, changamoto zinazoendelea kutafutiwa ufumbuzi na zile zitakazojitokeza, ni muhimu kuzitambua mapema, kuzijadili kwa uwazi na umakini ili kuzitafutia ufumbuzi kwa manufaa ya pande zote mbili za Muungano. Hivyo, ni imani yangu kuwa kusainiwa kwa Hati hizi leo, kutaongeza tija na hamasa ya kutafuta ufumbuzi wa hoja zilizobakia kwa ustawi wa Muungano wetu.
Ndugu Wajumbe, nawapongeza tena kwa jitihada za kuhakikisha Muungano wetu adimu na adhimu unaendelea kuimarika. Tuongeze jitihada katika kuzitafutia ufumbuzi hoja zilizobakia ambazo zipo katika hatua mbalimbali za kuzitafutia ufumbuzi. Naziagiza Wizara za Fedha na Mipango za SMT na SMZ kuchukua jitihada za makusudi kuzitafutia ufumbuzi hoja zinazohusu ushirikiano katika masuala ya fedha ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi.
Aidha, nasisitiza kwa sekta zote kuendeleza vikao vya kisekta kwa pande zote mbili za Muungano ili kupunguza hoja zinazoletwa kwenye kamati ya Pamoja.
Ndugu Wajumbe, baada ya maneno haya machache natamka rasmi kuwa, hoja za Muungano kumi na moja (11) zilizopatiwa ufumbuzi zimeondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.