Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Makampuni ya The Pula Group Dkt. Mary Stith katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Kampuni ya The Pula Group ni Kampuni ya Kimarekani inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya risasi (graphite) hapa nchini ambayo ni moja ya malighafi muhimu katika uzalishaji wa betri. Pamoja na mambo mengine mazungumzo hayo yalijikita katika kujadili masuala mbalimbali muhimu katika kutangaza fursa kwa lengo la kuvutia wawekezaji wengi zaidi katika sekta hiyo.
Akizungumza baada ya mkutano huo Dkt. Mary ameeleza sambamba na kumshirikisha Waziri Mulamula kuhusu mchango na nafasi ya Kampuni yake katika kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini hasa kwenye sekta ya madini pia ametumia fursa hiyo kujifunza na kupata uzoefu wa masuala mengi kuhusu Wanawake na Uongozi kutoka kwa Waziri Mulamula.
“Wakati huu ambao Dunia inakabiliana na adhari za madiliko ya Tabianchi, mahitaji ya madini ya ghraphite ambayo ni muhimu katika uzalishaji wa nishati ya umeme yameendelea kuongezeka Duniani kwa sababu ni rafiki kwa mazingira, nafarijika kuona Tanzania ikiwa na kiasi kikubwa cha hifadhi ya madini haya yenye viwango vya kimataifa” Amesema Dkt. Mary.
Aidha Waziri Mulamula kwa upande wake amemwakikishia Dkt. Mary kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi madhubuti wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini sambamba na kudumisha ulinzi na usalama.
Kampuni ya The Pula Group ilianza kuendesha shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini ya graphite nchini mwaka 2014.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanyamazungumzo na Balozi Mteule Prof. Adelardus Kilangi katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam. Prof. Adelardus Kilangi aliteuliwa kuwa Balozi Septemba 12, 2021.
Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameshiriki Sherehe ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Peace Corps Tanzania yaliyofanyika kwenye viunga vya Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam. Maadhimisho hayo yaliongozwa na kauli mbiu “Miaka Sitini ya Huduma na Urafiki”.
Akizungumza katika Maadhimisho hayo Waziri Mulamula ameeleza kuwa Tanzania ina thamini sana jitihada na mchango wa Marekani katika maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi kwenye maeneo mabalimbali hapa nchini ikiwemo; afya, elimu, miundombinu, maji, teknolojia ya habari na mawasiliano, kuimarisha demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria na utawala bora.
Waziri Mulamula aliongeza kusema wakati huu ambao nchi hizi mbili zinasherekea Maadhimisho ya Miaka Sitini ya Huduma na Urafiki, ni fursa nyingine ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana kutokana na ushirikiano wetu ambayo ni chachu katika kudumisha na kuimarisha ushirikiano wa karibu zaidi baina ya Nchi hizi mbili rafiki. Aidha, Waziri Mulamula amewashukuru Raia wa Marekani ambao kwa muda mrefu wamejitolea kufanya kazi bila kuchoka katika maeneo mbalimbali ya vijijini nchini wakishirikiana na Washirika wa ndani ikiwemo kufundisha hesabu na sayansi katika shule za upili, wakufunzi wa walimu katika teknolojia ya habari na mawasiliano na sekta ya afya.
“Nitumie fursa hii kusisitiza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Marekani na itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Peace Corps Tanzania katika kuleta maendeleo endelevu kwa Nchi yetu”. Alisema Waziri Mulamula.
Peace Corps Tanzania ni Taasisi ya Kimarekani inayochangia nguvu kazi katika shughuli
mbalimbali za maendeleo ya Kijamii na Uchumi kwa kujitolea. Kazi na majukumu ya Peace Corps Tanzaniayanaongozwa na Mkataba uliosainiwa kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marekani Januari 9, 1979.
Maadhimisho hayo pamoja na washiriki wengine yalihudhuriwa na Mhe. Dr. Donald Wright Balozi wa Marekani nchini Tanzania na Bi. Stephanie Joseph de Goes Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps Tanzania