Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 05 Oktoba, 2021 amekutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Uchumi Afrika (Arab Bank for Economic Development in Africa – BADEA) Dkt. Sidi Ould Tah, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Ould Tah amemshukuru Rais Samia kwa kuzungumza nae na kumhakikishia kuwa BADEA itaendelea kuunga mkono jitahada za Serikali ya Tanzania katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Aidha, Dkt. Ould Tah ameutambulisha mkakati mpya wa BADEA 2030 ambao unaainisha fursa zitokanazo na ongezeko la mtaji kutoka kwa wanahisa wake na kuwezesha kuongezeka kwa utoaji wa misaada na mikopo kwa mwaka.
Dkt. Ould Tah amesema mkakati huo unajikita kwenye miundombinu, vijana na wafanyabishara wadogo na wa kati, kuongeza mnyororo wa thamani katika kilimo, biashara na sekta binafsi pamoja na kuwajengea uwezo wahusika wa miradi hiyo.
Kwa upande wake Rais Samia ameishukuru BADEA kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika miradi ya maendeleo na utaalamu kwa zaidi ya miaka 40.
Aidha, Mhe. Rais Samia ameishukuru BADEA kwa kuonyesha fursa zilizopo katika mkakati wao mpya unaoendana na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III), unaolenga kuongeza ufanisi na ushindani kwa kuimarisha miundombinu, biashara, sekta binafsi pamoja na kuwajengea uwezo vijana na wafanyabishara wadogo na wa kati.