Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la wakazi wa Magomeni Kota la kununua nyumba zilizojengwa na Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) katika eneo hilo kwa kutoa maelekezo kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuruhusu wakazi hao kununua nyumba hizo kwa utaratibu wa Mpangaji-Mnunuzi kwa kurejesha fedha ya ujenzi pekee bila gharama ya ardhi.
Rais Samia ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua nyumba 644 zilizopo katika eneo la Magomeni Kota na kueleza kuwa kama ilivyoahidiwa na mtangulizi wake Hayati Dkt. John Joseph Magufuli wakazi hao wataishi miaka mitano bure na kwa miezi mitatu ya awali hawatachangangia gharama za huduma jumuishi.
Ad
”Nimeridha kuwa baada ya miaka mitano wananchi wa Magomeni Kota kuuziwa nyumba hizi kwa utaratibu wa Mpangajii-Mnunuzi na kurejesha gharama za ujenzi pekee, hatutawatoza gharama ya ardhi kwa sababu tukifanya hivyo mtashindwa kuzinunua.” Amesema.
Aidha amesema, kwa wakazi ambao wapo tayari kulipa gharama za ununuzi wa nyumba hizo wanaruhusiwa kulipa kidogo kidogo bila riba huku wakiendelea kuishi katika makazi hayo. Kuhusiana na utunzaji wa mradi huo Rais Samia amewataka wakazi hao kuzingatia usafi na kudumisha upendo na mshikamano
”Ninawaomba mtunze mradi huu kwa kuzingatia usafi wa nyumba hizi ambao ni dhamana yenu kwa sasa, nyumba kama hizi tunategemea mpikie gesi hatutegemei mpikie kuni katika maghorofa haya.” Amesema.