TANZANIA KUISAIDIA MSUMBIJI KUKOMESHA VITENDO VYA KIGAIDI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania itandelea kuwa mstari wa mbele kuisaidia nchi ya Msumbiji katika kukabiliana na vitendo ya kigaidi katika nchi hiyo.
 
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Machi 24, 2022) alipomuwakilisha Rais  Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa kujadili usalama katika eneo la Kusini Mashariki mwa Afrika hususan nchini Msumbiji na maeneo ya jirani (Aqaba Process), uliofanyika katika mji wa Aqaba uliopo nchini Jordan.
 
“Tanzania tutaendelea na ushiriki wetu wa kuisaidia Msumbiji kwa kiwango wanachohitaji, lengo ni kuhakikisha tunauondoa kabisa ugaidi nchini humo, tunapunguza hatari ya magaidi kuingia nchini Tanzania, pamoja na kuwasaidia kwa hali na mali wananchi wake kuendelea na shughuli zao”.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi katika mkutano wa kujadili usalama kwenye eneo la Kusini Mashariki mwa Afrika hususan nchini Msumbiji na maeneo jirani uliofanyika Machi 24, 2022 kwenye mji wa Aqaba nchini Jordan. Katikati ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Mbarouk Nassor Mbarouk.


Amesema kuwa mkutano huo pia umepokea mapendekezo mbalimbali kutoka kwa Msumbiji na wadau wa Aqaba Process kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano na kuisaidia Msumbiji kukabiliana na changamoto za ugaidi.
 
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “Eneo linaloshambuliwa ni Kaskazini mwa Msumbiji ambalo ni Kusini mwa nchi yetu, hivyo ushiriki wetu umekuwa ni muhimu sana”.
 
Mkutano huo ambao umeitishwa na Mfalme Abdullah II wa Jordan, utakuwa wa tatu  kufanyika tangu  kuanzishwa kwake mwaka 2015 na huwakutanisha viongozi wakuu wa nchi  za ukanda  wa Mashariki ya Afrika  kwa lengo la kujadili changamoto za ugaidi na namna ya kuudhibiti.
 
Baadhi ya viongozi walioshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, Rais  wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi

Ad
Ad

Unaweza kuangalia pia

Serikali ya Tanzania na Czech Zakubaliana Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili

Serikali za Tanzania na Czech kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kuvutia uwekezaji kati yao. Kuondoa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *