- Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Wananchi wanaoishi pembezoni mwa Miundombinu ya Barabara Nchini kuwa walinzi kwa kutoa Taarifa kwa vyombo husika dhidi ya wale wanaoharibu kwa makusudi miundombinu hiyo iliyojengwa kwa gharama kubwa.
- Alisema wapo baadhi ya Watu waliojitoa mshipa wa fahamu kwa kuiba alama zilizowekwa Bara barani, kuchimba Mchanga au udongo pembezoni mwake jambo ambalo kama Wananchi hawatakuwa tayari kutoa ushirikiano wao kwa vyombo vya Dola ile azma ya Serikali ya kuimarisha Sekta ya Mawasiliano inaweza kufifia.
- Balozi Seif Ali Iddi alitoa kumbusho hilo wakati wa hafla ya kuizindua rasmi barabara ya Kilomita Tatu iliyojengwa kwa Kiwango cha Lami kuanzia Wawi -Mabaoni hadi Mgogoni Chake Chake Pemba ikiwa ni mwanzoni mwa Shamra shamra za Maadhimisho ya kusherehekea Miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
- Alisema uzoefu unaonyesha wazi kwamba mahala popote palipojengwa Miundombinu ya Bara bara katika kipindi kifupi hutoa fursa kwa Wananchi wake kuimarika Kiuchumi kutokana na harakati za Kibiashara zinazoambatana na ujenzi wa Makaazi bora yanayolingana na uwepo wa Bara bara husika.
Ad