RAIS WA ZANZIBAR DKT. SHEIN ATOA SALAMU ZA MWAKA MPYA 2019

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi  wa Zanzibar kuendelea kuidumisha hali ya amani na utulivu ambayo ndio msingi wa mafanikio yanayoendelea kupatikana hivi sasa na yatakayopatikana hapo baadae.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika risala yake ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2019 aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, Ikulu mjini Zanzibar.
Rais Dk. Shein alisema kuwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya mwaka 2018 mafanikio makubwa yamepatikana ambayo yamechangiwa na kuwepo kwa amani, mshikamano, umoja na mapenzi yaliopo.
Katika risala yake hiyo Rais Dk. Shein alieleza kuwa hali ya amani, umoja na mshikamano uliopo nchini ni jambo muhimu linalowavutia Washirika wa maendeleo ambao wanaridhika na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ndio maana wanaiunga mkono katika mipango yake ya maendeleo.
Alisema kuwa hapana shaka kwamba iwapo amani, usalama na utulivu vitadumishwa na kufanya kazi kwa bidii Washirika wa Maendeleo watakuwa pamoja na Zanzibar katika kuisaidia ili kuweza kutekeleza malengo yaliyopangwa.
Rais Dk. Shein alitoa shukurani kwa wananchi wote kwa kuunga mkono juhudiza serikali za kuiletea maendeleo Zanzibar na kueleza kuwa moyo wao huo wa umoja na mshikamano umewezesha kuimarisha vizuri hali ya uchumi wa Zanzibar.
Hata hivyo, Dk. Shein alitoa shukurani nyingi kwa wananchi wote kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuiletea maendeleo Zanzibar ambapo moyo wao huo wa umoja na mshikamano umewezesha kuimarisha vizuri hali ya uchumi wa Zanzibar.
“Tukiwa tunaukaribisha mwaka mpya wa 2019, nachukua fursa hii kwa niaba ya wananchi wote  wa Zanzibar kuwashukuru kwa dhati  Washirika wetu wa Maendeleo kwa kuendelea kutuunga mkono, tunathamini mikopo, misaada na ushauri tulioupata kutoka kwao”, alisema Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa wakati unakaribishwa mwaka 2019 ni wajibu wa kila Taasisi ya Serikali ikajipima namna inavyoendelea kutekeleza mambo yaliyoagizwa katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015-2020.
“Nawakumbusha viongozi wenzangu viongozi wenzangu wote wa CCM tuliochaguliwa na wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, uliorudiwa mwezi Machi, 2016. Kadhalika jukumu hili wanapaswa walizingatie na wale wote niliowateua katika nyadhifa mbali mbali”,alisema Dk. Shein katika risala yake hiyo.
Katika risala yake hiyo Rais Dk. Shein alizitaja kumbukumbu za matukio yalitokea katika mwaka 2018 ikiwa ni pamoja na utiaji wa saini wa Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia (PSA), baina ya Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia na kampuni ya RAK GAS ya Ras Al Khaimah.
Aliongeza kuwa tukio jengine la kihistoria ni kufanyika kwa Tamasha la Utalii la Kimataifa ambalo lilihudhuriwa na Makampuni 150 ya Utalii ya ndani na nje ya nchi ambalo lilileta mafanikio katika kuwaunganisha wafanyabiashara wa utalii wa Zanzibar na wale wa Kimataifa na kuitangaza Zanzibar katika masoko ya Kimataifa.
Alieleza kuwa mwaka 2018 umefungua milango katika utekelezaji wa dhamira ya kuendeleza kilimo cha mpunga kwa njia ya umwagiliaji maji na utumiaji wa zana za kisasa ambapo tarehe 6 Disemba, 2018 Serikali ilitiliana saini Mkataba wa Ujenzi wa Miundombinu ya Kilino cha Umwagiliaji maji na Kampuni ya Kokon Hansol JV ya Jamhuri ya Korea kupitia Shirika la Maendeleo la nchi hiyo.
Pia, Rais Dk. Shein alieleza kuwa katika lengo la kuungana na nchi nyengine katika kuendeleza uchumi wa Bahari tarehe 26 hadi 28 aliongoza Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wa Kimataifa uliofanyika Nairobi nchini Kenya.
Alisisitiza kuwa kwa upande wa Zanzibar inauanza mwaka 2019 ikiwa imejipanga kwa kutafuta njia bora za kutumia rasilimali za bahari kwa kuitumia vizuri bahari ya Hindi iliyoizunguka kwani hili ni eneo muhimu kwa uchumi wa Zanzibar.
Akieleza jambo jengine muhimu ambalo limefanyika katika mwaka 2018, Rais Dk. Shein alisema kuwa tukio linalohusu jitihada za Serikali za kuwakinga wanawake wa Zanzibar na janga la saratani ya shingo ya kizazi ambapo mnamo April 10 Mama Mwanamwema Shein alizindua rasmi Mpango wa Chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Saratani ya Shingo wa Kizazi.
Vile vile, tarehe 5 Disemba 2018 alizindua Mpango wa Miaka Minne wa Uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya Kizazi ambao unawajumuisha wanawake wenye umri wa miaka 21 hadi 65 kazi ambayo itafanywa kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Jamhuri ya Watu wa China ambapo huduma zote pamoja na matibabu zitatolewa bure.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar inasifika kwa uzuri wake, historia yake na khulka nzuri za watu wake na hali ya usalama iliyopo ambapo Serikali nayo inafanya jitihada za kuhakikisha kwamba sifa njema ya Zanzibar ya kuwa ni sehemu salama yenye utulivu inaendelea kwua ni kichocheo cha kuwavutia wageni, watalii na wawekezaji sambamba na kurahisiha utekelezaji wa mipango ya kamedneleo.
Hivyo, mnamo tarehe 3 Novemba 2018 ulizinduliwa rasmi  Mradi wa Ulinzi wa Mji Salama ambao lengo lake ni kuhakikisha hali ya usalama kwa kutumia CCTV na vyombo vyengine vya kisasa ambapo dhamira ni kuendeleza mradi huu katika Mikoa mengine ya Unguja na Pemba hatua kwa hatua.
Licha ya mafanikio hayo yaliopatikana mwaka 2018, Rais Dk. Shein alieleza kuwa bado kunahitajika kuzidisha mapambano dhidi ya udhalilishaji wa wanwake na watoto na unyanyasaji wa kijinsia kwa vile kesi za vitendo hivyo bado zinaendelea kuripotiwa kwenye maeneo mbali mbali.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliwaahidi wananchi wote kwamba wale wote watakaobainika kwamba wamehusika kwenye tukio la uvujaji wa mitihani ya kidato cha Pili kwenye sekta ya elimu watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aliongeza kuwa tukio hilo ni la kusikitisha, linalokwenda kinyume na mipango ya maendeleo ya elimu ambalo halijengi mustakbali mwema wa elimu kwa watoto na kuwataka wananchi kujifunza athari za tukio hilo kwa Serikali, Wizara, Walimu, Wazazi, Wanafunzi na nchi kwa jumla.
Akimalizia risala yake hiyo, Rais Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wote kushiriki kwa wingi katika shughuli mbali mbali za kuadhimisha miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 zitakazofanyika katika maeneo yao kwani hizo ni sherehe zao kila mmoja ahakikishe anashiriki ipasavyo katika hatua zote.
Ad

Unaweza kuangalia pia

KAMPUNI YA SIGARA TANZANIA(TCC) KUTOA MSAADA WA VIFAA MBALIMBALI KWA WATU WENYE ULEMAVU ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba utayari wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *