DKT. KALEMANI AITAKA TANESCO KUENDELEZA MIRADI YA UMEME VIJIJINI

  • Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendelea kusambaza umeme vijijini mara wakandarasi wa umeme vijijini wanapomaliza kazi kwa mujibu wa mkataba.
  • Dkt. Kalemani aliyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji umeme vijijini katika Wilaya za Mpwapwa na Bahi mkoani Dodoma ambapo aliambatana na Wawakilishi wa wananchi katika maeneo hayo, Watendaji wa Wizara ya Nishati, TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
WAZIRI
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akikata utepe kuashiria uzinduzi wa umeme katika Kijiji cha Chinoje wilayani Mpwapwa. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene. Kulia kwa Waziri ni Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje.
  • “Yapo maeneo ambayo yalishasambaziwa umeme kutoka zamani kupitia miradi ya usambazaji umeme vijijini hivyo kazi ya TANESCO ni kuendelea kusambaza umeme kwenye maeneo hayo kwa muda wote badaala ya kuyaacha tu yakikosa umeme.” alisema Dkt Kalemani.
  • Akiwa kwenye wilaya hizo, Dkt Kalemani aliwasha umeme katika Kijiji cha Igoji na Chinoje vya wilayani Mpwapwa, pia aliwasha umeme katika Kijiji cha Chikola kilichoko wilayani Bahi na kuahidi umeme utawaka tarehe 12 Mei, 2019 katika Kijiji cha Chipanga wilayani Bahi.
  • Akizungumzia kazi za usambazaji umeme katika wilaya hizo mbili alisema kuwa, Wilaya ya Bahi ina vijiji 59 ambapo vijiji 19 tayari vimeshasambaziwa umeme na vijiji 40 vilivyosalia vinasambaziwa umeme kupitia mradi  wa REA wa Awamu  ya Tatu.
  • Aidha kwa Wilaya ya Mpwapwa alisema kuwa, Wilaya hiyo ina Vijiji 113ambapo Vijiji 78 tayari vimesambaziwa umeme huku kazi ya usambazaji umeme ikiendelea kwenye Vijiji vilivyosalia.
WAZIRI
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizungumza katika Kijiji cha Chinoje wilayani Mpwapwa kabla ya kuwasha umeme katika Kijiji hicho. Wa kwanza kulia ni Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene.
  • Akizungumza na wananchi katika Vijiji hivyo, Dkt Kalemani aliwaagiza Mameneja wa TANESCO kwenye Wilaya hizo kuhakikisha kuwa wanafungua vituo kwa ajili ya kuhudumia wananchi badala ya wananchi kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma TANESCO.
  • Kuhusu wakandarasi wa umeme vijijini wanaosuasua katika kazi zao, Dkt Kalemani alisema kuwa Serikali itachukua hatua kali dhidi yao hivyo ni vyema wakaongeza kasi katika utekelezaji wa kazi walizopewa na Serikali.
  • Kwa upande wake, Mbunge wa Kibakwe, George Simbachwene pamoja na kupongeza Wizara ya Nishati kwa ufuatiliaji wa karibu wa miradi  ya umeme vijijini alitoa ombi kwa Serikali kuhakikisha wakandarasi wa umeme vijijini wanasambaza umeme kwa wigo mkubwa  na pale mkandarasi anapomaliza muda wake TANESCO waendelee na kazi ya kusambaza umeme kwa wananchi.
  • Vilevile alisema kuwa, kazi ya upangaji wa vijiji au vitongoji vinavyopaswa kupelekewa umeme ushirikishe wawakilishi wa wananchi ili kuboresha utaratibu wa usambazaji umeme na hivyo kuepusha malalamiko yanayoweza kutokea kwa baadhi ya vijiji au vitongoji kuona kuwa vimerukwa bila sababu za msingi
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *