WAZIRI KALEMANI ATIMIZA AHADI YAKE KUWAWASHIA UMEME WANANCHI WA MWAKITOLYO

 

 • Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ametimiza ahadi yake aliyoitoa mwanzoni mwa mwezi huu (Juni) kwa wananchi wa Kijiji cha Mwakitolyo, Shinyanga Vijijini, kuwa umeme utawashwa katika eneo lao kabla ya Julai, 2019.
 • Dkt. Kalemani alitimiza ahadi hiyo jana, Juni 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi mkoani Shinyanga, ambapo aliwasha rasmi umeme katika jengo la Ofisi ya Serikali, Kitongoji cha Mwakitolyo Namba Tano.
UM
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (aliyeinua mkono), akifurahi na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kukata utepe kuashiria uwashaji rasmi wa umeme katika Kijiji cha Mwakitolyo, Shinyanga Vijijini, Juni 29, 2019.
 • Akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara kijijini Mwakitolyo, Waziri Kalemani alisema Serikali inatambua umuhimu na kuthamini mchango wa wachimbaji wadogo wa madini katika uchumi wa nchi.
 • Alisema, ndiyo maana aliagiza mchakato wa kupeleka umeme eneo hilo uharakishwe; baada ya kufanya ziara katika eneo hilo awali na kushuhudia wachimbaji wadogo wa madini wakifanya kazi zao bila umeme,
 • Kuhusu Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini (REA) katika eneo hilo, ambaye katika ziara yake ya awali, Waziri aliagiza kushikiliwa kwa Hati za kusafiria za Wakurugenzi wa Kampuni husika; kutokana na kusuasua kwa kazi, aliruhusu mmoja kati yao arejeshewe hati hiyo baada ya kuridhishwa na maendeleo ya kazi.
 • “Maendeleo ya kazi yao kwa sasa yanaridhisha. Naagiza Kiongozi wao mkuu, arejeshewe Hati yake lakini wenzake watatu wataendelea kuwepo hapa hadi watakapokamilisha kazi ya kuunganisha vitongoji vyote vya Mwakitolyo,” alielekeza Waziri.
UM
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kata ya Mwakitolyo, Shinyanga Vijijini, muda mfupi kabla ya kuwasha rasmi umeme katika eneo hilo, Juni 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi.
 • Aidha, Dkt. Kalemani alitoa maagizo kwa Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi FedGrace Shuma pamoja na Mkandarasi husika, kukamilisha kazi ya kusambaza nguzo za umeme katika eneo hilo ndani ya Wiki mbili tu ili eneo lote liwashwe umeme katika kipindi hicho.
 • Waziri alitoa rai kwa wananchi wa Mwakitolyo kujitokeza kwa wingi na kuendelea kulipia gharama ya kuunganishiwa umeme ambayo ni shilingi 27,000/- tu. Aidha, aliwataka viongozi wanaosimamia Taasisi mbalimbali za Umma na Miradi ya kijamii, kutenga fedha katika bajeti zao na kulipia gharama hiyo ndogo ili Taasisi na Miradi husika iunganishiwe umeme.
 • Awali, akikagua maendeleo ya kazi ya kuunganisha umeme katika Kijiji cha Mahembe, Waziri Kalemani aliuagiza uongozi wa TANESCO Shinyanga, kufunga Transfoma kubwa yenye uwezo wa kilovoti 200, kwenye Kituo cha Afya katika eneo hilo, ndani ya siku Tano, ili kuboresha huduma kwa wananchi.
 • Akizungumza katika ziara hiyo, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba, alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwapelekea wananchi maendeleo, hususani umeme vijijini.
UM
Fundi kutoka Kampuni ya Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini (REA), Kampuni ya Angelique International Limited ya India, akikamilisha zoezi la kuunganisha umeme katika Kitongoji cha Mwakitolyo Namba Tano, Shinyanga Vijijini wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) Juni 29, 2019. Wanaoshuhudia ni wananchi wa eneo hilo.
 • Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga, Donald Magesa, alisema uongozi na wanachama wa CCM mkoani humo, wanafurahi kuona Ilani ya Chama Tawala ikitekelezwa kwa vitendo.
 • “Ilani ya Chama inasema umeme uende kila nyumba. Tunatekeleza. Nawaombeni wananchi tujitokeze kwa wingi kulipia shilingi 27,000 ili kila mmoja apate umeme na tupate maendeleo kama Serikali inavyokusudia,” alisema Katibu.
 • Kwa upande wao, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwakitolyo, Nuhi Shomi na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwakitolyo Namba Tano, Benedict Robert, kwa nyakati tofauti, walimpongeza Waziri Kalemani, kutimiza ahadi aliyoitoa kwa wananchi wa eneo hilo kwa kuwashiwa umeme ndani ya muda mfupi.
 • Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani alifuatana na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama Tawala na wataalamu mbalimbali kutoka Wizarani, REA na TANESCO.Na Veronica Simba – Shinyanga
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *