Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa, mradi wa matumizi ya gesi majumbani ambao utazinduliwa hivi karibuni katika mkoa wa Mtwara utasaidia kuepuka matumizi ya mkaa ambao licha ya kuharibu mazingira, husabisha maradhi mbali mbali.
Alisema hayo, Septemba 14, 2019 kwa nyakati tofauti wilayani Kibiti, Mkoa wa Pwani, alipokuwa akizungumza na wananchi katika vijiji vya Mangwi na Njopeka, wakati alipoenda kushiriki katika tukio la kukabidhi vifaa tiba kwa Zahanati ya Mangwi na mfano wa hundi ya shilingi milioni 19,480,000 kwa shule ya msingi Njopeka vilivyotolewa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa Tatu kushoto) akimkambidhi mfano wa Hundi, Mwalimu Mkuu wa Shule Msingi Njopeka (wa Nne kulia) ambayo imetolewa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Wa Pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt James Mataragio.
Naibu waziri, alitoa wito kwa wananchi watakaopitiwa na mradi huo kutumia gesi katika shughuli zao mbali mbali za kila siku majumbani hali itakayopunguza matumizi ya mkaa na kutunza mazingira na kwamba mradi huo unatarajiwa kufika hadi katika wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani.
Vilevile, Naibu Waziri aliipongeza TPDC kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kusimamia sekta ya Mafuta na Gesi nchini na jitihada zao zimewezesha masuala mbalimbali ikiwemo kupelekea asilimia 50 ya umeme nchini kuzalishwa kwa kutumia Gesi Asilia.
“Niwapongeze pia kwa kusimamia vyema bomba la Gesi linalozewesha gesi kusafirishwa mpaka Dar es Salaam na kuanza kusambazwa kwa matumizi ya majumbani, pia limewezesha kupata umeme mwingi ambao sasa tunausambaza hadi vijijini kupitia mradi wa REA na TANESCO.” Alisema Mgalu
Naibu Waziri wa Nishati,, Subira Mgalu (kulia) akikabidhi vifaa vya tiba kwa Zahanati ya Kijiji cha Mangwi wilayani Kibiti. Wa Pili kulia ni Mbunge wa Kibiti Ally Ungando. Wa Tatu kutokaa kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt James Mataragio.
Wananchi wa vijiji hicho walimpongeza Naibu Waziri kwa jitihada mbalimbali anazofanya ili kuleta maendeleo kupitia nyanja mbali mbali na kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili.
Akiwa wilayani humo, Naibu Waziri aliwasha umeme katika Kijiji cha Kingwira ambapo aliwasihi waatalamu ambao wanafanya kazi za wiring kupunguza bei ili kila mwananchi aweze kumudu gharama.
‘Serikali imewatengenezea mazingira wezeshi, imewapa kazi, wapunguzieni gharama wananchi ili waweze kumudu gharama. ’’alisema Mgalu
Naibu Waziri pia alisisitiza kuhusu suala la nguzo kutolipiwa katika miradi ya umeme vijijini na kuwapongeza Mameneja wa TANESCO wanaohakikisha kwamba agizo hilo la Serikali linatekelezwa.