MIRADI YA KIMKAKATI YA UMEME ITAKAYOFIKISHA MW 10,000 MWAKA 2025 YATAJWA

  • Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt Tito Mwinuka ameeleza kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo inalenga kutimiza adhma ya Serikali ya kuwa na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
2-01
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mbele kulia) pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua (mbele kushoto) wakiwa katika kikao na Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara mara baada ya kumaliza kikao chao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
  • Taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo ameitoa tarehe 23/10/2019 katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika jijini Dodoma ambapo Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliiongoza Wizara ya Nishati katika uwasilishaji wa taarifa hiyo akiwa ameambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Hamisi Mwinyimvua na Menejimenti ya Wizara pamoja na Taasisi zake.
  • “Wizara ya Nishati kupitia TANESCO inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya umeme ikiwemo ya kuzalisha umeme, usafirishaji umeme katika msongo mkubwa na usambazaji lengo likiwa ni kukidhi mahitaji ya umeme yanayoongezeka  na miradi hii itakapokamilika itachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa sekta ya umeme.” Alisema
4-01
Wataalam kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati wakiwa katika kikao na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani) pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua (hayupo pichani) mara baada ya kumaliza kikao chao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
  • Dkt. Mwinuka alitaja miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (MW 2115) ambao mkandarasi ameanza rasmi utekelezaji wake tarehe 15 Juni, 2019 kwa kuanza ujenzi wa bwawa pamoja na njia ya kuchepusha maji ambapo mpaka sasa uchorongaji wa handaki la mchepuko wa maji unaendelea na matarajio ya kumaliza mradi huo ni Juni 2022.
  • Alitaja mradi mwingine wa kimkakati kuwa ni mradi wa kuzalisha umeme  wa Rusumo (MW 80) ambao kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 55 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020.
  • “ Mradi mwingine tunaoutekeleza ni mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia wa Kinyerezi I Extension (MW 185) ambao upo katika hatua za mwisho za utekelezaji kwani umefikia asilimia 84 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020.” Alisema Dkt. Mwinuka
3-01
Wataalam kutoka Wizara ya Nishati wakiwa katika kikao na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani) pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua (hayupo pichani) mara baada ya kumaliza kikao chao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
  • Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO alitaja miradi mingine ya kuzalisha umeme wa maji ambayo ipo katika hatua za awali za utekelezaji kuwa ni mradi wa Ruhudji (MW 358), Mradi wa Kakono (MW 87), mradi wa Rumakali (MW 222), mradi wa Malagarasi (MW 45) na mradi wa Kikonge (MW 300).
  • Aidha, aliongeza kuwa, mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia ambao upo katika hatua za awali za utekelezaji ni mradi wa Mtwara ambao utazalisha  megawati 300.
  • Wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge walitoa maoni mbalimbali yatakayosaidia kuboresha sekta ya umeme nchini ambayo Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliahidi kuwa yatafanyiwa kazi.
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *