WAZIRI KALEMANI AKAGUA UJENZI WA KITUO CHA KUPOZA UMEME BULYANHULU NA KUTOA MAELEKEZO

  • Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, Desemba 4, 2019 amekagua maendeleo ya ujenzi unaolenga kupanua kituo cha kupoza umeme Bulyanhulu, wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga na kutoa maelekezo kadhaa kwa uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na mkandarasi husika.
  • Akiwa amefuatana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha, viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa pamoja na wataalam kutoka wizarani, TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Waziri alimwagiza Mkandarasi kukamilisha ujenzi husika ifikapo Mei, 2020.
2-01
Ujenzi kwa ajili ya upanuzi wa kituo cha kupoza umeme Bunyanhulu, wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga ukiendelea. Taswira hii ilichukuliwa Desemba 4, 2019 wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), kituoni hapo.
  • Alisisitiza kauli hiyo na kusema kuwa muda hautaongezwa hata siku moja, hivyo akamtaka Meneja wa TANESCO mkoani humo kumsimamia mkandarasi ili akamilishe kazi kwa wakati na viwango stahiki.
  • “Hii ni kazi muhimu sana hivyo lazima ikamilike kwa wakati.”Tunapanua kituo hiki ili kukiongezea uwezo kutoka megawati 16 za sasa hadi kufikia megawati 51. Ujenzi ni mkubwa maana utahusisha pamoja na mambo mengine, kujenga njia ya kusafirisha umeme umbali wa kilomita 57 kutoka Bulyanhulu hadi Geita.”
3-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akiwahamasisha wananchi wa kijiji cha Igunda, wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga (hawapo pichani), kuiga mfano wa bibi Teresia Shotoo (kulia kwa Waziri), aliyelipia shilingi 27,000 na kuunganishiwa umeme kwenye nyumba yake. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi wilayani humo, Desemba 4, 2019.
  • Aidha, alieleza kuwa, ujenzi utakapokamilika, kituo hicho kitasaidia kufua na kupitisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 unaotoka Shinyanga kwenda hadi Geita ambako pia kunajengwa kituo kingine kikubwa cha megawati 100.
  • Akifafanua zaidi, Waziri alisema ujenzi wa kituo cha Geita pamoja na upanuzi wa kituo cha Bulyanhulu, gharama yake ni takribani dola za kimarekani milioni 23 na kwamba mradi unahusisha pia kupeleka umeme kwenye vijiji 10 kutoka Bulyanhulu kupitia Busanda hadi Buseresere.
4-01
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha (kushoto), akimweleza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia), hali ya upatikanaji umeme wilayani humo. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi wilayani Kahama, Desemba 4, 2019.
  • Katika hatua nyingine, Waziri aliuagiza uongozi wa TANESCO wilayani humo, kuhakikisha vifaa mbalimbali vinavyotumika kuendeshea mitambo katika kituo hicho cha kupoza umeme cha Bulyanhulu, vikiwemo vikata umeme maarufu kama ‘circuit breaker’ vinabadilishwa mara kwa mara badala ya kusubiri hadi viharibike, suala ambalo limekuwa likisababisha kukatika kwa umeme.
  • Vilevile, aliagiza ujenzi wa ofisi na nyumba ya kuishi wahudumu wa kituo hicho, uanze mara moja ili kuwawezesha watumishi hao kuishi karibu na kituo, waweze kutoa huduma mara moja pindi linapotokea tatizo kwenye mitambo.
5-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya ujenzi unaohusisha upanuzi wa kituo cha kupoza umeme Bulyanhulu, Desemba 4, 2019.
  • Awali, Waziri alitembelea kijiji cha Igunda wilayani humo, ambapo aliwasha rasmi umeme, Pia, alitembelea kijiji cha Ntobo, Kata ya Msalala na kuwaeleza wananchi kuwa umeme utafikishwa katika kijiji hicho hivi karibuni. Veronica Simba – Kahama
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.