RAIS MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA DARAJA LA KIGONGO – BUSISI LENYE UREFU WA KM 3.2

 • Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi lenye urefu wa kilometa 3.2 na upana wa mita 28.45 ambalo litakalounganisha mawasiliano ya barabara kati ya Mikoa ya Mwanza na Geita kukatiza Ziwa Victoria.
 • Sherehe za uwekaji jiwe la msingi zimefanyika katika eneo la Kigongo, Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza na kuhudhuriwa na wananchi na viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera, Wabunge, viongozi wa taasisi mbalimbali, viongozi wa Dini na viongozi wa vyama vya siasa.
m14-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa na msichana Salma Yasini, Kiongozi wa wanafunzi wa Shule ya msingi ya Iseni B ambaye amemkabidhi shilingi milioni tano ukiwa ni mchango wake kusaidia ujenzi wa vyoo na madarasa shuleni hapo wakitokea kwenye sherehe za uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Kigongo-Busisi lenye urefu wa Kilomita 3.2 kwenye sherehe iliyofanyika Kigongo jijini Mwanza leo Desemba 7, 2019.
 • Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.66 umepangwa kukamilika mwezi Julai 2023 kwa gharama ya jumla ya shilingi Bilioni 699, fedha zote zinatolewa na Serikali ya Tanzania.
 • Daraja hilo refu kuliko yote Afrika Mashariki, na la 6 kwa urefu Barani Afrika litakuwa mbadala wa vivuko vya MV Misungwi, MV Sengerema na MV Mwanza, na litajengwa kwa teknolojia ya madaraja marefu inayoitwa Extra Dosed Bridge ambapo litajengwa juu ya nguzo 67 zikiwemo nguzo 3 zenye urefu wa meta 40 na umbali wa meta 160 kutoka nguzo moja hadi nyingine.
m12-01
Mbunge wa Misungwi Mhe Charles Kitwanga akishiriki kwenye ngoma ya utamaduni ya kucheza na nyoka mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli wakati wa sherehe ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa Kilomita 3.2 kwenye sherehe iliyofanyika Kigongo jijini Mwanza leo Desemba 7, 2019
 • Mhandisi Mfugale amebainisha kuwa daraja hilo linalojengwa na wakandarasi China Civil Engineering Construction Corporation na China Railway 15 Group Corporation litaondoa adha ya usafiri wa wananchi, mizigo na magari ambayo kwa sasa huvushwa kwa vivuko, na kwamba baada ya ujenzi idadi ya magari yanayovuka kwa siku inatarajiwa kuongezeka kutoka 1,600 hadi 10,200 kwa siku na muda kuvuka utapungua kutoka saa 2:30 hadi dakika 4.
m11-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akipiga ngoma kwa furaha wakati wa sherehe za uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Daraja la Busisi-Kigongo lenye urefu wa Kilomita 3.2 kwenye sherehe iliyofanyika Kigongo jijini Mwanza leo Desemba 7, 2019
 • Akizungumza katika sherehe hizo, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Kanda ya Ziwa hususani Mikoa ya Mwanza na Geita kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo litakuwa utatuzi wa kero ya miaka mingi, iliyosababisha vifo kutokana na ajali za majini na wagonjwa kucheleweshwa hospitali, kuchelewa kwa biashara na safari za wananchi, na kwamba kukamilika kwake kutakuwa chachu ya kukua kwa uchumi wa kanda hiyo na Tanzania kwa ujumla.
m10-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiangalia picha kubwa ya mfano wa Daraja la Busisi-Kigongo lenye urefu wa Kilomita 3.2 baada ya kuweka jiwe la msingi na kuzindua rasmi kuanza kwa ujenzi wake kwenye sherehe iliyofanyika Kigongo jijini Mwanza leo Desemba 7, 2019
 • Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amesema kuanza kwa ujenzi wa daraja hilo ni uthibitisho kuwa Tanzania sio masikini na kwamba tukiamua tunaweza, hivyo ametoa wito kwa Watanzania wote kutembea kifua mbele kwa kuwa daraja hilo litaharakisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
 • Amewataka wakandarasi wanaojenga daraja hilo kufanya kazi usiku na mchana ili waweze kumaliza ujenzi kabla ya muda uliopangwa kwa kuwa Watanzania wanalihitaji daraja hilo haraka, na ametoa wito kwa wananchi wa Mwanza na Geita kujitokeza kupata ajira katika kazi za ujenzi, kuuza bidhaa mbalimbali vikiwemo vyakula na amewakumbusha Watanzania wote kuendelea kulipa kodi kwa kuwa mradi huo pamoja na miradi mingine ya ujenzi wa reli, barabara, majengo, maji, afya na umeme inatekelezwa kwa fedha za Watanzania wenyewe.
m9-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa na viongozi mbalimbali akikata utepe kuanzisha rasmi kwa Ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa Kilomita 3.2 kwenye sherehe iliyofanyika Kigongo jijini Mwanza leo Desemba 7, 2019
 • Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale kwa mchango wake mkubwa wa kusanifu madaraja makubwa, madaraja madogo na barabara, jukumu ambalo anaendelea nalo kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
 • Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Aloyce Kamwelwe amesema pamoja na ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi, Serikali imejenga madaraja makubwa 77 na madaraja madogo 8,020 na kwamba ujenzi wa madaraja mengine makubwa 6 unaendelea ambayo ni Wami (Pwani), Magara (Manyara), Sukuma (Mwanza), Kitengule (Kagera), Msingi (Singida), Ruhuhu (Ruvuma) na Selander (Dar es Salaam).
m8-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akisaidiwa na Spika wa Jamhuri ya Muungano Mhe Job Ndugai akifunua kitambaa kuashiria uwekaji rasmi wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa Kilomita 3.2 kwenye sherehe iliyofanyika eneo la Kigongo jijini Mwanza leo Desemba 7, 2019
 • Spika wa Bunge, Mhe. Job Yustino Ndugai amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali ya Awamu ya Tano kuandika historia nyingine kubwa ya kujenga daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki na ameahidi kuwa Bunge litaendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kupitisha fedha za ujenzi wa mradi huo na miradi mingine ya maendeleo katika bajeti ya Serikali.
m4-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiangalia picha kubwa ya mfano wa Daraja la Busisi-Kigongo lenye urefu wa Kilomita 3.2 baada ya kuweka jiwe la msingi na kuzindua rasmi kuanza kwa ujenzi wake kwenye sherehe iliyofanyika Kigongo jijini Mwanza leo Desemba 7, 2019
 • Tarehe 08 Desemba, 2019 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Mwanza kwa kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa meli na chelezo katika ziwa Victoria.
Ad

Unaweza kuangalia pia

LIVE: UZINDUZI WA MAJENGO YA OFISI YA MANISPAA NA MKUU WA WILAYA KIGAMBONI JIJINI DSM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11, Febuari, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.