RC WANGABO AILILIA MV LYEMBA KUHUDUMIA WANANCHI ZIWA TANGANYIKA

  • Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameishauri Mamlaka ya Bandari nchini kuona umuhimu wa kuifufua MV Lyemba ambayo ilikuwa ikitoa huduma ya kubeba mizigo na abiria katika ziwa Tanganyika ambapo kwa sasa hakuna hata meli moja inayotoa huduma ya kubeba abiria katika ziwa hilo linalounganisha mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma na nchi za jirani ikiwemo Zambia pamoja na Jamhuri ya Demokrasia ya watu wa Congo.
1-01
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili toka kushoto) alipotembelea mzani wa Barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga kusikiliza changamoto za wafanyakazi wa mzani huo waliodai kuwa magari mengi huepuka mzani huo na hatimae kukosesha mapato serikali.
  • Wangabo amesema kuwa hali ya usafiri katika ziwa tangayika sio nzuri ni mbaya kutokana na wananchi kupanda majahazi, mitumbwi na bodi ambapo mara kadhaa wamekuwa wakijazana jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa Maisha ya wananchi hao.
  • “Hili jambo hili Mamlaka ya Bandari pamoja na vyombo vuingine vinavyohusika mfanye haraka sana kwakweli ile meli ya MV Lyemba kwakweli ni mkombozi katika hili ziwa Tanganyika kwasababu hakuna chombo kingine kikubwa mbacho kinaweza kikasaidia hawa wananchi pamoja na mizigo yao watu wanahangaika sana na ni miaka sasa imekuwa ni muda mrefu, miaka kadhaa imekwishapita kwahiyo hili mlipaswa mlione hata kwa jicho la huruma basi,” Alisema
2-01
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa mbele) pamoja na wataalamu wengine wakitoka eneo ambalo kumetokea mmeguko wa ardhi (landslide) katika kipande cha mwisho cha barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga hali inayokwamisha umaliziaji wa barabara hiyo iliyobaki Km 1 kuisha.
  • Na kuonya kuwa isifike hatua watu wakapoteza Maisha kwenye Ziwa Tanganyika ndipo ije kuonekana kuna umuhimu wa kuokoa Maisha ya watu wakati wamekwishaangamia na kuwataka wachukulie jambo hilo kwa uzito mkubwa kabla ya kupoteza maisha ya watu wanaoishi katika mwambao wa ziwa hilo.
  • Mh.Wangabo ameyasema hayo alipofanya ziara katika Tarafa ya Kasanga kujionea maendeleo ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa km 107 kutoka Sumbawanga – Matai – Kasanga ambapo imekamilika kwa asilimia 97 pamoja na bandari ya Kasanga ambayo imekamilika kwa asilimia 50 akiwa pamoja na wajumbe wa kamati ya usalama ya mkoa pamoja na wataalamu kutoka Mamlaka ya Bandari pamoja na Wakala wa wa Barabara nchini.
3-01
Bandari ya Kasanga.
  • Aidha, akitoa taarifa kwa niaba ya Meneja wa Badari hizo za Ziwa Tanganyika Yudas Suwanyi alisema kuwa kuna meli kadhaa zinazohudumu katika ziwa hilo ambazo hubeba mizigo peke yake ikiwemo meli ya MV malagalasi inayomilikiwa na Mtanzania inayofanya safari zake kutegemeana na upatikanaji wa mizigo katika mikoa hiyo.
  • Wakati akitoa taarifa ya uboreshaji wa bandari hiyo ya Kasanga kaimu mhandisi wa bandari za ziwa Tanganyika Nyakato Lwamnana amesema kuwa pamoja na maboresho ya majengo kadhaa ikiwemo nyumba za watumishi, jengo la kusubiria abiria, maghala, ofisi kadhaa pia kuna upanuzi wa gati unafanyika ambapo kwa sasa kuna gati la urefu wa mita 20 lenye uwezo wa kupokea meli moja na kupanuliwa hadi kuwa na urefu wa mita 120 na kuweza kuchukua meli mbili kwa wakati mmoja ili kuepuka changamoto ya kusubiriana.
4-01
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiendelea kukagua ujenzi wa upanuzi wa gati ya bandari ya Kasanga.
  • “Gharama za mradi ni 4,000,764,000/=, ambapo ulianza tarehe 29.4.2019 mradi ni wa mwaka mmoja mpaka tarehe 28.4.2020 tunategemea mradi huu kukamilika kwasasa umefikia asilimia 50 na muda ambao umekwishapita ni asilimia 76 kama mnavyoona muda mrefu umepita kuliko utekelezaji utekelezaji tuko asilimia 50,” Alisema.
  • Kwa upande wake meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROAD) mkoani Rukwa Mhandisi Masuka Mkina alisema kuwa imebaki changamoto ndogo ya kupotomoka kwa udongo (landaslide) ili kuweza kukamilisha barabara hiyo iliyoanza kujengwa tarehe 13.1.2010 ambapo hadi kufikia tarehe 31.12.2019 ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 97 na kwa bajeti ya mwaka 2019/2020 serikali imetenga shilingi bilioni 5.8 kumalizia ujenzi huo unaotarajiwa kumalizika mwezi June, 2020.
6-01
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akiongea na mafundi wanaoendelea na ujenzi wa upanuzi wa gati ya Bandari ya Kasanga kutoka mita 20 hadi mita 120 ili kuwa na uwezo wa kupokea meli mbili kwa wakati mmoja.
  • “Wanampango wa kumleta mtaalamu kusudi aweze kufanya upembuzi wa eneo hili halafu awape muongozo wa nini kifanyike, namna ya kujenga eneo hili ambalo udongo umeporomoka, wamesema wameshampata Kampuni ya Noro Plan Tanzania ndio mshauri ambae atakuja kufanya utafiti hapa kujua chanzo na nini cha kufanya,” Alieleza.
  • Katika ziara hiyo Mh. Wangabo na timu yake pamoja Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Rukwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa Ndg. Enos Budodi waliridhishwa na maendeleo ya mradi huo na kuwataka wananchi kutumia fursa zinazopatika kutokana na kukamilika kwa miradi hiyo ya kimkakati ya mkoa.
Ad

Unaweza kuangalia pia

MRADI WA UJENZI WA MIUNDOMBINU BANDARI YA KABWE MKOANI RUKWA WAKAMILIKA KWA ASILIMIA 85

Ujenzi wa mradi wa miundombinu katika Bandari ya Kabwe mkoani Rukwa ambao unagharimu Sh.bilioni 7.498 …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *