“TULINDE TABAKA LA OZONI” – MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachewene akizungumza katika Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni akimuwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maadhimisho haya yamefanyika Jijini Dodoma na yameenda sambamba na utoaji wa zawadi kwa washindi wa insha kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Hifadhi ya Bioanuai kwa wanafunzi wa Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya Elimu ya Juu.

Tanzania imepunguza zaidi ya tani 216 sawa na asilimia 86 ya kiasi cha matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni azma ikiwa ni kuondosha matumizi ya kemikali hizi kufikia mwaka 2030.

Haya yamesemwa hii leo Jijini Dodoma na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuadhimishia Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni kupitia Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene.

Ad

Alisema, katika jitihada za kuhifadhi Tabaka la Ozoni, mwaka 1996, Serikali ya Tanzania iliandaa na kutekeleza Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni ili kuhakikisha kwamba hakuna sekta ya uchumi au jamii inaathirika kutokana na matakwa ya Itifaki ya Montreal. Aidha, programu hii ilianzisha utaratibu wa kusimamia na kudhibiti  uingizaji wa kemikali na bidhaa zenye kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni kutoka nje ya nchi.

Kwa upande mwingine Mheshimiwa Makamu wa Rais aliikumbusha jamii wajibu wa kuendelea kulinda tabaka la ozoni kwa kuepuka kuingiza nchini kemikali na vifaa vinavyotumika kumong’onyoa tabaka la ozoni kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika (mtumba) bali kuingiza nchini vipoozi mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachewene akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa Insha kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Hifadhi ya Bioanuai. Washindi hao ni kutoka Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya Elimu ya Juu. Hafla hii imefanyika katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma. Wengine katika picha ni Balozi Joseph Sokoine Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Vumilia Nyamoga Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Bw. Faraja Ngeregeza Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira – Ofisi ya Makamu wa Rais.

Na Lulu Mussa, Dodoma.

“Natoa rai kwa jamii kununua bidhaa zilizowekwa nembo ya “Ozone friendly” yaani ‘sahibu wa Ozoni’ au “CFC-free” ikiashiria haina wala haikutengenezwa na kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni, kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani ama vifaa vya kuzima moto vyenye kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni” Alisisitiza Makamu wa Rais.

Maadhimisho ya mwaka huu yalienda sambamba na utoaji wa zawadi kwa washindi wa inshakuhusu mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya bioanuai kwa ngazi za Shule ya Msingi, Sekondari na Vyuo vya Elimu ya Juu kwa lengo la kukuza na kupima uelewa, kuhamasisha ubunifu kwa wanafunzi na vijana kuhusu mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya bioanuai.

Pia alitoa wito kwa washirika wa maendeleo kuunga mkono jitihada za kutunza mazingira katika: kuhifadhi tabaka la ozoni; kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi; kuhifadhi bioanuai na usafi wa mazingira. Pia, kuhusisha vijana wadogo na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za mazingira ili kuwa na kizazi chenye uelewa na kinachothamini hifadhi ya mazingira.

Awali, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine alisema juhudi za kulinda Tabaka la Ozoni zinaendelea kupata mafanikio duniani na kusisitiza kuwa huenda litarejea katika hali yake ya awali takribani miaka 30 mpaka 50 ijayo endapo hapatakuwa na kemikali haribifu zitakazoingia tena angani. “Juhudi zozote za kupunguza matumizi ya kemikali hizo zitaleta matokeo ya manufaa kwenye kurejesha tabaka la Ozoni katika hali ya kawaida. Juhudi za kila mmoja wetu zinatakiwa ili kupunguza na kuondosha madhara katika Tabaka la Ozoni yanayosababishwa na shughuli zetu tunazofanya” alisisitiza Balozi Sokoine.

Ozoni ni tabaka la hewa lililopo kwenye angahewa ya juu, takribani kilometa 15 hadi 30 juu ya ardhi likiwa na kazi ya kuchuja kiwango kikubwa cha mionzi ya jua isifike kwenye uso wa dunia. Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya ni “Miaka 35 ya Kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa manufaa ya afya ya binadamu na mazingira” (Ozone for Life35 years of Ozone Layer Protection). Kaulimbiu hii inatukumbusha umuhimu wa kulinda na kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa kupunguza uzalishaji na matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa Tabaka hili.

Ad

Unaweza kuangalia pia

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA WOMENLIFT HEALTH

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Maelezo kutoka kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *