TANZANIA IMETAJWA KAMA NCHI YA KIELELEZO CHA AMANI NA DEMOKRASIA KATIKA BARA LA AFRIKA

Norway yaitaja Tanzania kama kielelezo cha amani na demokrasia katika chaguzi Barani Afrika kutokana na mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu unavyofanyika kwa amani,utulivu na usawa kwa wagombea wa vyama vyote huku wananchi wakijitokeza kwa wingi kusikiliza sera za wagombea.

Balozi wa Norway nchini Tanzania Balozi Elisabeth Jacobsen ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi na kuongeza kuwa maandalizi ya uchaguzi mkuu yamefanyika kwa kufuata taratibu za kisheria huku tume ya Taifa ya Uchaguzi ikishughulikia baadhi ya malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya vyama vya siasa na wadau mbalimbali jambo ambalo linaifanya Tanzania kuwa kinara wa demokrasia katika mchakato mzima wa uchaguzi. 

Ad
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Kabudi akimuonesha Balozi Norway nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen moja ya kipengele cha sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi wakati alipokuwa akimkabidhi nakala ya nyaraka hizo

Pamoja na masuala ya kisiasa Balozi huyo amesema katika mazungumzo yao wamegusia pia masuala ya ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi hususani katika suala la elimu,afya,nishati na uwekezaji pamoja na biashara baina ya nchi hizo mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amemuomba Balozi huyo wa Norway kuendelea kushirikiana na Tanzania na kumshukuru kwa Nchi hiyo kukubali kutoa kiasi cha dola za marekani milioni 7 kwa ajili ya mradi wa TASAF jambo litakalosaidia kupunguza umasikini kwa watanzania hususani katika kipindi hiki ambapo nchi nyingi zimeathiriwa na janga la Corona. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Kabudi akikagua nakala za hati za utambulisho za Balozi mteule wa Uswisi hapa nchini Mhe. Didier Chassot

Mbali na Balozi huyo wa Norway pia Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sweden hapa nchini Balozi Anders Sjöberg ambapo amezungumzia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi,haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari na kuvipongeza vyombo vya habari hapa nchini kwa kuandika habari za wagombea wa vyama vyote bila ya ubaguzi na ameonesha kufurahishwa kwake na mwitikio wa wananchi katika mikutano ya kampeni na kuomba maamuzi ya wananchi katika sanduku la kura yaheshimiwe.

Kuhusu suala la haki za binadamu prof. Kabudi amesema taswira inayotolewa kuhusu suala hilo haiakisi hali halisi iliyopo nchini na kwamba Tanzania inaheshimu na kulinda misingi ya haki za binadamu kiasi cha suala hilo kuingizwa katika ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi ili kikiingia madarakani kitekeleze na kulinda misingi hiyo. 

Balozi wa Sweden nchini Mhe. Anders Sjöberg akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati alipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam

Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amepokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Uswis hapa Nchini Mhe. Didier Chassot.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Je! Wajua Mchango wa Madini ya Tanzanite katika Pato la Taifa?

Madini ya Tanzanite, yanayopatikana pekee katika eneo dogo la Mererani, Tanzania, ni miongoni mwa rasilimali …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *