MRADI WA UMEME RUSUMO UNA MANUFAA MTAMBUKA KWA WATANZANIA – SERIKALI

Veronica Simba – Ngara

Serikali imeeleza kuwa Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kagera, unaotekelezwa Rusumo wilayani Ngara, una manufaa mtambuka kwa Watanzania.

Ad

Hayo yalielezwa jana, Septemba 28, 2020 na Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi huo ikihusisha Wakurugenzi wa Bodi na Kamati ya Ufundi, wakiwa katika ziara ya kazi yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia Mradi husika.

Sehemu ya majengo ya Kituo cha Afya Rusumo, kilichoko wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, kinachojengwa kupitia Mradi wa Umeme wa Rusumo unaotekelezwa wilayani humo. Taswira hii ilichukuliwa Septemba 28, 2020 wakati wa ziara ya Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi huo, kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia Mradi husika.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Kiongozi wa Timu hiyo, Mhandisi Innocent Luoga ambaye ni Mjumbe wa Bodi wa Kamati husika, alisema mbali na umeme, Mradi huo utawanufaisha Watanzania kupitia miradi mbalimbali ya kijamii ambayo alisema iko katika hatua nzuri za utekelezaji.

Mhandisi Luoga ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati alieleza kuwa miradi ya kijamii inayotekelezwa ni pamoja na inayohusu sekta za afya, elimu, maji, mifugo na kilimo.

Akizungumzia lengo la Timu hiyo ya Serikali kutembelea miradi ya kijamii inayoendelea kutekelezwa, Mhandisi Luoga alisema ni kujionea hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wake, kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi ili kuwezesha miradi hiyo kukamilika kwa wakati.  

Baadhi ya wajumbe wa Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo wakijadiliana jambo nje ya Zahanati ya Kijiji cha Kyenda, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera baada ya kufanya ukaguzi katika Zahanati hiyo wakiwa katika ziara ya kazi, Septemba 28, 2020. Kutoka kulia ni Kiongozi wa Msafara, Mhandisi Innocent Luoga ambaye ni Kaimu Kamishna kutoka Wizara ya Nishati na Mjumbe wa Bodi ya Mradi huo, Mhandisi Salum Inegeja kutoka Wizara ya Nishati na Mhandisi Costa Rubagumya kutoka TANESCO ambao ni wajumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mradi.

“Tumetembelea shule za msingi na sekondari, zahanati, vituo vya afya na miradi ya maji ambayo yote inayotekelezwa hapa Ngara na tumejiridhisha kuwa kwa sehemu kubwa imefkia hatua nzuri na baadhi yake imekamilika.”

Hata hivyo, alieleza kuwa Timu yake imebaini changamoto ya baadhi ya miradi kusuasua hususan Mradi wa Maji unaotekelezwa Rusumo ambao umechelewa kutokana na kukosekana vibali vya ujenzi.

Alisema yeyé na wenzake wametatua changamoto husika kwa kuelekeza vibali hivyo vipatikane haraka ili Mkandarasi aanze kazi na kukamilisha Mradi kwa wakati.

Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikikagua nyumba ya kuishi walimu katika Shule ya Sekondari Mumiterama, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera iliyojengwa kupitia Mradi huo. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo Septemba 28, 2020.

Aidha, kwa miradi mingine inayosuasua inayohusu majengo ya shule na vituo vya afya, Timu iliwataka wakandarasi husika kukamilisha kazi kwa wakati, kuzingatia viwango na ubora.

Kuhusu manufaa ya umeme, Mhandisi Luoga alieleza kuwa Mradi wa Rusumo utakapokamilika utazalisha megawati 80 ambazo zitagawanywa kwa nchi tatu zinazohusika ambazo ni Tanzania, Rwanda na Burundi kwa kila moja kupata megawati 27.

Alisema kuwa kwa upande wa Tanzania, Mradi utasaidia kuongeza umeme katika gridi ya Taifa pamoja na kuboresha hali ya upatikanaji nishati hiyo katika Mkoa wa Kagera.

 “Kama alivyoelekeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli, kuwa Mkoa wa Kagera uingizwe katika gridi ya Taifa, hivyo kukamilika kwa Mradi wa Rusumo kutawezesha hilo.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Luteni Kanali Michael Mtenjele, akizungumza na Timu hiyo ofisini kwake kabla ya kuanza ziara, alipongeza kazi nzuri inayoendelea kufanyika ambayo alisema imeleta manufaa makubwa kwa wananchi wake.

Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikikagua tanki la maji linalojengwa katika Kitongoji cha Ngome, Kijiji cha Kasulo, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera kupitia Mradi huo, Septemba 28, 2020. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo.

“Miundombinu ambayo imejengwa ni ya kipekee. Hatukuzoea kuona Shule za Msingi zinakuwa na Jengo la Utawala lakini kupitia Mradi huu hilo limefanyika na kwakweli inapendeza sana,” alifafanua.

Naye Mratibu wa Miradi ya Maendeleo ngazi ya Wilaya, Herman Hume alieleza kuwa miradi hiyo ya kijamii inayoendelea kutekelezwa wilayani Ngara ilitengewa fedha kiasi cha dola milioni tano za Marekani ambazo ni sawa na takribani shilingi bilioni 12 za Tanzania.

Wengine wanaoshiriki katika ziara hiyo itakayoendelea kwa siku mbili nyingine ni Mhandisi Salum Inegeja kutoka Wizara ya Nishati na Mhandisi Costa Rubagumya kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mradi wa Rusumo.

Pia, Timu imefuatana na Mhandisi Patrick Lwesya, Meneja Mradi wa Rusumo, Gaspar Mashingia, Afisa Mwandamizi, Jamii, Maendeleo na Uhamaji Makazi pamoja na Maafisa kadhaa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ngara.

Ad

Unaweza kuangalia pia

“Nani aliyeunda Jumuiya ya Madola na kwa nini?”

Malkia Elizabeth II pamoja na mawaziri wake wakuu wa Jumuiya ya Madola mwaka 1962. Picha: …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *