NAIBU WAZIRI BYABATO, APONGEZA UJENZI WA KITUO CHA UMEME WA 400KV SINGIDA

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amepongeza kasi ya ujenzi wa Kituo cha kupoza umeme wa 400kV cha Singida ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 94 na kinatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.

Wakili Byabato  alitoa pongezi hizo wakati wa ziara yake mkoani Singida, Februari 22, 2021, ya kukagua Kituo hicho na kuzungumza na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani humo, kwa lengo la kufahamiana, kusikiliza changamoto zinazowakabili pamoja na kutoa maelekezo ya kuboresha utendaji kazi wa shirika hilo.

Ad
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (kushoto) akionyeshwa namna ambavyo Kituo cha Kupoza Umeme cha Singida kinavyofanya kazi kupitia teknolojia ya kisasa, wakati wa ziara yake ya kukagua kituo hicho, iliyofanyika Februari 22, 2021, mkoani huo.

Aidha alisema kuwa kazi kubwa zote zinazohusufu mfumo wa umeme katika kituo hicho zimekamilika, na kinachoendelea sasa ni kukamilisha kazi ndogondogo ikiwemo ukarabati wa mazingira katika eneo husika.

“Nawapongeza sana wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa kituo hichi, wamejenga kwa kasi inayotakiwa, na inavyoonekana hapa wanaweza kukabidhi mradi huu kabla ya muda uliopangwa, hata watanzania wakiona kazi hii watafurahi na kuona fedha zao zinafanya kazi ipasavyo ya kuwaletea maendeleo kwa haraka zaidi kupitia Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais wetu Dkt. John Magufuli”, alisema Wakili Byabato.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (kushoto) akionyeshwa namna ambavyo umeme wa 400kV, utakavyokuwa unaingia katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Singida wakati ziara yake ya kukagua kituo hicho, iliyofanyika Februri 22, 202, mkoani huo.

Nawasisitiza wawekezaji wa ndani na nje ya Tanzania, kuja kuwekeza mkoani Singida kwa kuwa mkoa huu una umeme mwingi zaidi ya mahitaji husika, wauhakika, wakutosha na ziada.

Aidha alisema kuwa mazingira ya uwekezaji ni salama na rafiki wakati wote kwa wenye viwanda, migodi na shughuli zote zinatohitaji umeme.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo, alipiga marufuku mahusiano ya kimapenzi sehemu za kazi kwa wafanyakazi na watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuwa yanaharibu na kuzorotesha utendaji kazi.

Alisema kuwa kujihusisha na mapenzi sehemu za kazi kunasababisha watumishi na wafanyakazi hao kufanya kazi pasipo kuzingatia sheria na maadili pamoja na weledi katika taaluma zao, pia ni kosa kisheria.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, akisoma maelezo yalioandikwa katika mashine umba zitakazotumika kwa umeme wa 400kV, katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Singida wakati wa ziara yake ya kukagua kituo hicho, iliyofanyika Februri 22, 2021 mkoani humo.

Alieleza wazi kuwa, wenye mahusiano sehemu za kazi wayahalalishe kwa kufunga ndoa, ili mmoja kati yao ahamishie ofisi nyingine kiutendaji kwa faida ya taasisi husika na familia kwa jumla.

“Marufuku mahusiano ya mapenzi kazini, ukiwa na mpenzi ofisini huduma zinazotorota, natoa mfano kiongozi akiwa na mahusiano msaidizi wake, lazima kazi zitalegalega na nyingine kutofanyika kabisa, mteja ama mtumishi mwingine atataka kuona na kiongozi husika au kufikisha ujumbe, lakini mpeleka ujumbe anaweza asiufikishe kwakuwa tu hataki mpenziwe asumbuliwe ama ashikwe na wivu, msikubali kazi kuharibiwa kwa starehe za wengine”, alisisitiza Wakili Byabato.

Wakili Byabato alifafanua kuwa, kwa wale watakaokuwa na mapenzi ya siri sehemu za kazi, wakibainika watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria za kazi nchi.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (katikati) akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Singida,(hawapo pichani), kulia ni Kaimu Meneja Mwandamizi,Kanda Kati, Mhandisi Cecilia Msangi, kushoto ni Mwakilishi wa Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Edson Ngabo, wakati wa ziara ya Naibu Waziri huo mkoani humo, Februari 22,2021.

Halikadhalika alipiga marufuku kwa watumishi hao kujihusisha na vitendo vya rushwa na kueleza kuwa baadhi ya watumishi wamekuwa wakiweka mazingira ya kupewa rushwa ili kutekeleza majukumu yao.

Alitaja miongoni mwa mazingira wanayotengeza watumishi hao ili wapate rushwa, kuwa ni pamoja na kutotimiza wajibu wao kwa wakati na kuchelewa kutoa huduma kwa wateja pamoja na kufanya uzembe.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, (katikati mbele suti ya blue) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Singida, wakati wa ziara yake mkoani humo, Februari 22, 2021.

Vilevile alitaka kila ofisi ya TANESCO nchini kutenga fungu maalum la fedha kwa ajili ya kuwapatia madereva pamoja na wahudumu wa ofisi zitakazowasaidia watu hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Alisema kuwa watumishi hao wamekuwa wakitumia fedha zao binafsi kufanya shughuli mbalimbali, akitolea mfano kwa madereva kuwa wamekuwa wakiziba pancha, kuosha magari nk.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *