Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani amewapongeza wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa kufanya kazi kwa ufanisi ambao umechagiza nchi kuingia katika uchumi wa kati kutokana na uwepo wa nishati inayotabirika.
Dkt.Kalemani ametoa pongezi hizo jijini Dodoma, tarehe 5 Mei, 2021 wakati akifungua Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Nishati ambapo Mkutano huo uliongozwa na Mwenyekiti, Kheri Mahimbali ambaye ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara, Mhandisi Leonard Masanja.
“Wizara ya Nishati ni injini katika uchumi wa Taifa letu, huwezi kuzungumzia maendeleo bila kugusa masuala ya nishati, na nishati si umeme tu, bali kuna gesi, mafuta na nyinginezo, ujenzi wa uchumi wa viwanda vikubwa na vidogo unategemea nishati kama vile ya umeme ambayo inachochea kwa haraka katika kujenga viwanda ambavyo vinasisitizwa katika uchumi huu wa kati.” Amesema Dkt.Kalemani
Ameongeza kuwa, utendaji mzuri wa wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake umepelekea wananchi wengi kutumia umeme ambapo kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanatumia nishati hiyo, na hii inatokana na juhudi zinazofanywa na wafanyakazi hao.
Mbali ya pongezi hizo, Waziri wa Nishati amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na usahihi wenye weledi ili kuendelea kupata mafanikio na kujenga uchumi imara.
Aidha, amewaasa kuendelea kudumisha ushirikino kati ya Mfanyakazi na Muajiri na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni ili kuongeza ufanisi.
Vilevile, amewasisitiza viongozi wa Wizara kuzingatia maslahi ya wafanyakazi ikiwemo kupandisha vyeo, madaraja na kulipa mafao ili kuwapa morali wafanyakazi ya kuchapa kazi zaidi.
Kwa upande wa wafanyakazi, alitoa angalizo la kutokufanya kazi kwa mazoea na badala yake kila mfanyakazi anapaswa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu, kujituma, kasi na kuzingatia viwango.
Kuhusu masuala ya kipaumbele ya kimkakati yaliyopangwa na Wizara, ikiwemo utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (MW 2115), ameagiza kuwa, yatekelezwe kwa wakati na Baraza la Wafanyakazi lihakikishe kuwa masuala hayo yanatekelezeka.
Aidha ameagiza kuwa, Baraza hilo lijadili na kutoa maoni kuhusu ufanikishaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya usambazaji umeme katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ya vijiji, miradi ya gesi ukiwemo wa Kuchakata na Usindikaji Gesi asilia (LNG), mradi wa Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki na ujenzi wa miundombinu ya umeme katika Reli ya Kisasa (SGR).
Teresia Mhagama, Dodoma
Dkt. Kalemani amesisitiza pia, kuhusu wananchi kupewa elimu ya matumizi ya umeme huku akitolea mfano kuwa kuna baadhi ya maeneo, Serikali inatumia fedha nyingi kupekeleka miradi ya umeme lakini wananchi wanaounga umeme si wengi kutokana na ukosefu wa uelewa wa matumizi ya nishati hiyo.
Awali, Mwenyekiti wa Mkutano huo, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, alisema kuwa Muundo wa Baraza hilo la Wafanyakazi lina wajumbe wapatao 50 wanaotoka makundi mbalimbali na kwamba baadhi ya kazi mahsusi za Baraza hilo ni kujadili na kupitisha mpango wa Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Alitaja baadhi ya kazi nyingine za Baraza hilo kuwa ni, kujadili taarifa ya utekelezaji wa miradi ya mafuta na gesi, miradi ya umeme na nishati mbadala inayoendelea pamoja na mipango ya maendeleo kwa mwaka 2021/2022.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUGHE, Tawi la Wizara ya Nishati, Zghambo Chinula, aliipongeza Serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Nishati na pia, alitumia fursa hiyo kueleza masuala mbalimbali yanayohusu Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati ikiwemo ya upandishaji madaraja na stahili mbalimbali.