Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Wazee wote nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ina dhamira ya dhati ya kushughulikia masuala mbalimbali yanayowahusu ili waweze kuishi maisha mazuri na salama.
Rais Samia ametoa ahadi hiyo tarehe 07 Mei, 2021 Mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na Wazee wa Dar es Salaam kwa niaba ya Wazee wote wa Tanzania baada ya kupokea risala yao iliyosomwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Mzee Salum Abdallah Matimbwa.
Katika risala hiyo Wazee hao wameomba kutatuliwa changamoto za matibabu, kutungwa sheria ya wazee, kupatiwa fursa za kiuchumi ikiwemo mikopo na misaada, kupatiwa pensheni, kuondolewa kero katika vyombo vya usafiri na kupatiwa nafasi katika vyombo vya maamuzi.
Rais Samia amewashukuru na kuwapongeza Wazee wote wa Tanzania kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kulilea Taifa kutokana na uzoefu na ujuzi walionao na pia amewashukuru kwa pongezi za kupokea kijiti cha Urais na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amewaahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itajitahidi kushughulikia changamoto walizozitaja kulingana na uwezo wa kifedha utakavyoruhusu lakini amemtaka Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima kushughulikia kwa haraka changamoto ya matibabu ya Wazee nchini kote.
Kuhusu pensheni kwa Wazee wote amesema kulingana na hali ya uchumi kwa sasa Serikali haitaweza kutekeleza ombi hilo mpaka hapo hali ya uchumi itakapoimarika lakini amesema imejipanga kuwawezesha Wazee kupitia mradi wa kusaidia kaya masikini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) na kwamba baada ya kuisha kwa mradi unaoendelea hivi sasa Serikali inajipanga kuendeleza mradi huo ili uwafikie wazee wote nchini.
Pamoja na kukubali kuwa Serikali itaimarisha nyumba za Wazee, Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa jamii kuendeleza utamaduni mzuri wa kuwatunza wazee vizuri na kwa upendo majumbani badala ya kuwaweka kwenye vituo vya wazee.
Aidha, ametoa wito kwa Wazee hao na Wazazi wote nchini kuwalea vijana wao katika maadili mema ili watambue wajibu wao kwa Wazee, nidhamu na heshima kwa jamii na kuwajali Wazee wote hasa wanapotumia huduma za kijamii ikiwemo mabasi ya abiria na sehemu za kutolea huduma.
Ameonya dhidi ya vitendo vya ujambazi na wizi vilivyoanza kujitokeza katika Mkoa wa Dar es Salaam na amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IJP-Simon Sirro kudhibiti vitendo hivyo mara moja.
Rais Samia amesema katika kutekeleza vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita anatarajia kuendeleza kazi nzuri iliyofanyika katika awamu zote za uongozi zilizopita, kumtumia Mtanzania yeyote mwenye ujuzi na maarifa ya kufanya kazi na atayeonekana anafaa ilimradi asiwe na dosari za kimaadili na usalama, na kutokana na hilo atafanya mabadiliko ya kitaasisi na uongozi kadiri atakavyoona inafaa kwa nia njema ya kulipeleka Taifa mbele.
Ameupongeza Mkoa wa Dar es Salaam kwa kukaribia kumaliza kabisa kero ya maji baada ya kukamilika kwa miradi miwili ya maji, ameahidi kuendeleza juhudi za kuongeza uzalishaji wa umeme ili utumike kuendeleza viwanda na kuuza nje ya nchi, kuongeza kasi ya kupanua huduma za mawasiliano kupitia mkongo wa Taifa, kusimamia uhuru, haki na demokrasia na kukuza uhusiano na ushirikiano na Mataifa mbalimbali duniani kama alivyofanya hivi karibu katika ziara yake rasmi nchini Kenya.
Rais Samia amewaomba Wazee wote nchini kumuunga mkono na kuwakumbusha Watanzania wote wajibu wao wa kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa, kulipa kodi na kusimamia maadili ya Kitanzania.
Mkutano huo umehudhuriwa na Makamu wa Rais Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Ndg. Philip Mangula, Viongozi wa Dini na viongozi wa vyama vya siasa.