Veronica Simba – Tabora
Serikali imewataka Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini kote kuheshimu makubaliano ya utendaji kazi yaliyoafikiwa baina ya pande hizo mbili kupitia mikataba waliyosaini.
Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo wakati akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo Mkoa wa Tabora, Septemba 8 mwaka huu.
Kikao hicho kilikuwa ni sehemu ya ziara ya Bodi mkoani humo kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Wakili Kalolo aliyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi husika iliyobainisha kuwa baadhi ya Wakandarasi wanasuasua hivyo kuchelewesha kukamilika kwake, jambo lililo kinyume na mikataba yao ya kazi.
Akisisitiza, alisema Serikali kamwe haitamvumilia Mkandarasi yeyote mwenye utendaji kazi duni unaokwamisha miradi hiyo na kuwakosesha wananchi fursa ya kuboresha maisha yao kutokana na nishati ya umeme.
“Kitendo cha kukwamisha kwa kuchelewesha Mradi au kwa namna nyingine yoyote ni uhujumu uchumi. Naomba muelewe Serikali haitakubali hivyo hatutasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekwenda kinyume na Mkataba,” alisisitiza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mjumbe wa Bodi Oswald Urassa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga walitoa onyo kwa Wakandarasi wanaozembea kuheshimu Serikali ya Tanzania kwani iko thabiti na haina mzaha katika kusimamia miradi ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Katika hatua nyingine, Ujumbe huo wa Bodi ulitembelea maeneo mbalimbali mkoani humo ambako utekelezaji wa miradi ya umeme unaendelea na kuzungumza na viongozi wa vijiji na vitongoji ili kusikia maoni yao.
Akitoa maoni kwa Bodi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Igalula wilayani Uyui, Athumani Ramadhani alisema wananchi katika eneo hilo wameupokea Mradi wa Umeme Vijijini kwa furaha na matumaini.
“Wananchi wameanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mashine za kusaga. Pia tunashukuru maana umeme huu haukatiki-katiki. Ombi langu kwa Serikali wananchi wote wafikishiwe nishati hii,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigwa wilayani Uyui, Hussein Maganga aliishukuru Serikali kwa kubuni miradi ya umeme vijijini akiielezea kuwa imekuwa yenye manufaa makubwa kwa wananchi kwani imechangia kuboresha maisha yao.
Bodi ya Nishati Vijijini inaendelea na ziara katika Mikoa mbalimbali nchini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Bodi hiyo ikiwa mkoani Mwanza Septemba 6 mwaka huu, iliagiza Mkandarasi Sagemcom anayetekeleza Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili A, kuandikiwa barua ya kumtaka akamilishe kazi kwa wakati vinginevyo hatua za kuvunja Mkataba wake zitachukuliwa.