Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mradi wa kuzalisha umeme wa kikanda wa Rusumo utakuwa mkombozi kwa wananchi wa mikoa ya Kagera, Kigoma , Rukwa na Katavi kwani utazalisha umeme wa uhakika utakaowezesha Mikoa hiyo kuunganishwa na gridi ya taifa.
Mradi huo unaotekelezwa kwa kuzingatia makubaliano ya Kiserikali ya nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi baada ya kuingia makubaliano rasmi mwaka 2012 na utazalisha Megawati 80 ambao kila Nchi mwanachama atapata Megawati 27.
“Mkakati wa Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni kuunganisha Mikoa yote kwenye gridi ya taifa, na sasa tumebakiwa na Mikoa minne ya Kagera, Kigoma, Katavi na Rukwa, huko kote kazi ya ujenzi wa laini za umeme ili kuiunganisha Mikoa hiyo unaendelea.” Alisema na kuongeza
Waziri Mkuu amesema Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia imedhamiria kuondoa changamoto ya umeme nchini kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya kuzalisha umeme pamoja na kuongeza vyanzo vya kuzalisha nishati hiyo ili kuhakikisha maeneo yote ya nchini yanapata umeme wa uhakika hususan maeneo ya vijijini.
Ameyasema hayo (Jumapili, Septemba 19, 2021) baada ya kukagua mradi huo wa uzalishaji wa umeme ulioko katika eneo Rusumo Wilayani Ngara Mkoani Kagera unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa gharama ya shilingi bilioni 82.
“Nimefarijika kwa hatua iliyofikiwa na kwamba kazi bado inaendelea, hatua mliyoifikia ni nzuri, inawezekana Mheshimiwa Rais Samia nae akaja kuona maendeleo ya mradi huu ili kuendelea kuwatia moyo na kuweka mkazo katika ukamilishaji wake.” Alisema
Waziri Mkuu ametoa wito kwa wakandarasi na wasimamizi wa mradi huo ambao hadi kufikia mwezi Julai, utekelezaji wa mradi kwa ujumla umefikia asilimia 81.2 ya utekelezaji kuongeza kasi katika ujenzi na kuepuka vikwazo ambavyo awali vilisababisha mradi huo kukamilika kwa wakati. “Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais ninapenda kutoa shukrani kwa wakandarasi na wasimamizi wote wa mradi huu”.
Aidha, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa mradi huo kwa Nchi zote tatu ni sehemu ya kuendeleza mahusiano mazuri baina ya Nchi hizo pamoja na kuendelea kudumisha undugu na ushirikiano, “Tanzania, Burundi na Rwanda ni Nchi rafiki na zimejenga ushirikiano wa muda mrefu na sisi sote ni ndugu na mradi huu unaendelea kuthibitisha undugu wetu, hivyo ni vyema tuendelee kuenzi Uhusiano huu.” Alisema.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati Mheshimiwa Stephen Byabato amesema mradi huo umetoa ajira 726 kwa Nchi zote tatu na Tanzania imepata nafasi 260 za ajira, na pia utakuwa ni kichocheo cha kuwepo kwa wawekezaji katika sekta ya viwanda ikiwemo uzalishaji wa madini ya Nickel kata ya Bugarama, Wilayani Ngara.
Mradi huo unatekelezwa kwa Muungano wa Wakandarasi wanne ambapo wawili kutoka China, CGCOC Group Ltd na Jiangxi Water & Hydropower Construction Company Ltd (CGCOC – JWHC JV) wanajenga bwawa la maji pamoja na miundombinu mingine; na muunganiko wa Wakandarasi Andritz Hydro GmbH ya Ujerumani na Andritz Hydro PVT Ltd ya India wanaohusika na ufungaji wa mitambo ya kuzalisha na kusambaza umeme.