Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, tarehe 21 Septemba, 2021 ameshiriki ufunguzi wa Mjadala Mkuu katika Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo Wakuu wa Nchi na Serikali walishiriki na kuanza kutoa hotuba zao.
Pembeni wa mkutano huo, Samia Suluhu Hassan, ameshiriki Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi na Serikali Wanawake wanaoshiriki mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kumhakikishia Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdulla Shahid kuwa Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kunakuwepo na usawa wa kijinsia licha ya vikwazo vinavyojitokeza.
Katika kikao hicho, Rais Samia ameeleza kuwa tangu amekuwa Rais ameendelea kuteua viongozi wanawake katika nafasi mbali mbali ambazo hazijawahi kushikwa na wanawake ili kuondokana na dhana ya kuwa kuna nafasi ambazo wanawake hawawezi.
“ Hivi karibuni nimemteua Waziri wa Ulinzi ambaye amekuwa mwanamke wa kwanza kushikilia nafasi hiyo nchini mwetu, ili kuondokana na dhana kuwa wanawake wanaweza nafasi fulani tu” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa hivi karibuni ameunda timu ya wataalamu ambayo kwa sasa wanaangalia namna bora kwa Tanzania kufanikiwa katika kupata usawa wa kijinsia wakati wa uongozi wake na timu hiyo itakuja na mapendekezo kadhaa ya kuwainua wanawake katika vita dhidi ya umaskini.
Maeneo ambayo timu hiyo inapitia ni pamoja na marekebisho ya sheria kandamizi, sera na mikakati ya kuwasaidia wanawake katika kupata fursa kwenye nyanja mbali mbali ikiwemo ajira, elimu na nyinginezo za kuwainua kiuchumi kama vile kumiliki ardhi,kupata mikopo na nafasi za uongozi.
Rais Samia pia ametoa wito kwa washiriki wenzake katika kikao hicho kutotoa fursa kwa ugonjwa wa virusi vya Korona, UVIKO – 19 kuwa kikwazo cha kuzuia mafanikio kwenye usawa wa kijinsia na kusisitiza kuwa ili Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu kufanikiwa, lengo namba 5 kuhusu usawa wa kijinsia ni lazima lifanikiwe.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Dunia Bw. David Malpass ambapo amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa jitihaza za kupambana na UVIKO 19 nchini Tanzania.
Aidha, Bw. Malpass amemhakikishia Rais Samia kuwa Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza uchumi kupitia mabadiliko ya kidijitali kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Kwa upande wake Rais Samia ameishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake kwa Tanzania katika huduma za jamii pamoja na mapambano dhidi ya UVIKO 19. Vilevile, Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), Bi. Ngozi Okonjo-Iweala ambapo viongozi hao wamezungumzia kuwezesha biashara kwa kuimarisha upatikanaji wa chanjo, usimamizi wa uvuvi na kilimo.