Na. Farida Ramadhani na Ivona Tumsime, WFM, Dodoma
Serikali imesema kuwa miradi yote mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa nchini imeshapangwa ndani ya bajeti za kisekta za Wizara husika ambazo hupitishwa na Bunge kila mwaka.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Wanamipango nchini kwa Mwaka 2020, jijini Dodoma.
Bw. James alitoa ufafanuzi huo baada ya kusambaa kwa taarifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa kuwa Serikali inakurupuka kuibua miradi ambayo haijulikani na haijapangiwa fedha za kuitekeleza.
“ Miradi inatekelezwa kwa mujibu wa bajeti inayopitishwa na Bunge ambayo inairuhusu Serikali kukopa ndani na nje ya nchi, kukusanya Kodi na kupokea misaada ili itekeleze bajeti yake”, alieleza Bw. Doto James.
Alisema kuwa baada ya bajeti kupitishwa kinachofuata ni utekelezaji wa bajeti ambapo Serikali hutumia fedha za makusanyo ya mapato, mikopo na misaada kwa mujibu wa sheria kwa kuwa Serikali haipokei fedha kiholela.
Bw. James alisema kuwa Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada inampa Waziri wa Fedha wajibu kutafuta fedha za utekelezaji wa bajeti iliyoridhiwa na Bunge.
Kwa upande wa utekelezaji wa mipango ya miradi Bw. James alisema kumekuwa na changamoto ya upatikanaji na utunzaji wa taarifa za miradi ambazo huwezesha maandalizi ya mipango na kufanya tathmini ya utekelezaji jambo lililosababisha Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kutengeneza Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo ili kutatua changomoto hiyo.
“Mfumo huo utakuwa na sehemu zote za mzunguko wa mradi yaani kuanzia uibuaji, ugharamiaji, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini, utoaji taarifa na ufungaji wa mradi baada ya utekelezaji kukamilika”, alieleza Bw. James.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na Mipango aliwaagiza wanamipango wote nchini kuongeza ubunifu katika kupanga mipango mbalimbali ya nchi ili kuiwezesha nchi kufikia malengo kwa wakati.
Alisema kutokana na hadhi ambayo Tanzania imefikia ya kuwa na Uchumi wa Kati, inabidi wanamipango wabadili namna ya kupanga na kutekeleza mipango ya nchi na kuwakumbusha kuwa suala sio kupanga tuu bali ni kupanga mipango inayotekelezeka na kuhakikisha inatekelezwa ipasavyo ili kupata matokeo yaliyokusudiwa.
Naye Kamishna wa Mipango ya Kitaifa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Nicolaus Shombe, alisema kuwa dhima ya Kongamano hilo ni Mipango ya Kujenga Uchumi Shindani Unaoongozwa na Mauzo Nje inayotokana na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Miaka Mitano unaotarajiwa kuanza mwaka 2021/22.
Kwa upande wa washiriki wa Kongamano hilo akiwemo Dkt. Joel Mmasa, wameahidi kushiriki kikamilifu kutoa maoni na ushauri utakaosaidia Serikali kuja na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Miaka Mitano pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22.
Aidha wameeleza kuwa watatumia maoni na ushauri utakaotolewa katika Kongamano hilo kupanga mipango itayowezesha nchi kupiga hatua zaidi katika hadhi ya Uchumi wa Kipato cha Kati na kuwa nchi ya kipato cha kati katika kiwango cha juu.