WIZARA YA MAWASILIANO YAWAKABIDHI WAKANDARASI MIKATABA YA SHILINGI BILIONI 7.5

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (wa tatu kulia) akishuhudia Makabidhiano ya mkataba ya kazi ya ujenzi, uwekaji na usimikaji wa majina ya mitaa/barabara na namba za nyumba katika halmashauri 12 nchini, baina ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula(wa tatu kushoto) na mwakilishi wa kandarasi ya Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) katika hafla iliyofanyika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma. Kulia Naibu Waziri Mhe. Mhandisi Kundo Mathew na Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Jim Yonazi.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile  amewaagiza wakandarasi wanaokwenda kutekeleza miradi minne ya miundombinu ya mawasiliano yenye thamani ya shilingi bilioni 7.5, kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hiyo ndani ya muda wa mkataba bila kuongeza hata siku moja ya ziada.

Dkt. Ndugulile alizungumza hayo alipokuwa katika hafla ya makabidhiano ya mikataba ya kazi hiyo baina ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula na wakandarasi hao wazalendo ambao ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Raddy Fibre Solution Ltd katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.

Ad
Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Zainab Chaula akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa kandarasi ya Raddy Fibre Solution Ltd, Ramadhani Hassani Mlanzi mkataba wa kazi ya ujenzi wa Miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma. Kulia ni Waziri wa Wizara hio Mhe.Dkt. Faustine Ndugulile na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi wakishuhudia. 

Miradi hiyo ni pamoja na  kujenga, kupanua na kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuunganisha na kuimarisha mawasiliano kutoka Mkoa wa Singida hadi Mkoa wa Mbeya, maeneo ya Mkoa wa Mtwara ili kuunganisha mawasiliano kati ya Tanzania na Msumbiji na kutoka eneo la Mji wa Serikali Mtumba hadi Msalato jijini Dodoma.

Aliongeza kuwa jumla ya kilomita 409 zitaunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika maeneo hayo na Halmashauri 12 nchini zitawekewa vibao vya majina ya mitaa/barabara na namba za nyumba katika kutekeleza Mradi wa anwani za makazi na postikodi.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (Kulia) akizungumza na wakandarasi, Menejimenti ya Wizara hiyo na waandishi wa habari katika hafla ya kuwakabidhi wakandarasi mikataba ya kazi ya ujenzi wa Miundombinu ya Mawasiliano baina ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula na wakandarasi hao katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma

Na Faraja Mpina- WMTH

Dkt. Ndugulile amesema kuwa lengo ni kuhakikisha mpaka kufikia mwaka 2025 asilimia 80 ya wananchi wanapata mawasiliano ya uhakika na kushiriki katika kuinua uchumi wa kidijitali kupitia biashara mtandao, ambapo mnunuzi na muuzaji lazima wawe na mawasiliano ya mtandao na mnunuzi kuwa na anwani ya makazi ili afikishiwe bidhaa aliyonunua mpaka nyumbani kwake.

“Sina shaka na wakandarasi wazalendo, mtajiengua ninyi wenyewe iwapo mtakuja na visingizio vya kutokamilisha kazi kwa wakati, mkafanye kazi mchana na usiku kuhakikisha miradi inakamilika ndani ya muda wa mkataba na ubora unaokubalika”, Dkt. Ndugulile

Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa Wizara inaendelea na mchakato wa kushughulikia suala la vifurushi na bando na kuomba wananchi kuwa na subira mpaka mwisho wa mwezi huu ili Wizara kuja na tamko rasmi ambalo halitaathiri mapato ya watoa huduma, mapato ya Serikali na vilevile kutomuathiri mwananchi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Ndugulile ametoa rai kwa wananchi wasipokee maelekezo yeyote kuhusu miamala binafsi kwa njia ya simu bali njia sahihi ni kwenda kwenye vituo vya mawakala vinavyotambulika na vilivyosajiliwa na makampuni ya simu.

“Tunataka kuimarisha mifumo ya mawakala wa makampuni ya simu ili kuweza kuwabaini na kuwachukulia hatua mawakala ambao sio waaminifu”, Dkt. Ndugulile

Amesema kuwa, Serikali imeanza mkakati wa kushughulika na watu wanaotoa lugha za matusi, kashfa na utapeli  mitandaoni ambapo mpaka sasa genge la watu 17 wanaoongoza genge la uhalifu mitandaoni waliokuwa wamejificha mkoani Morogoro wameshakamatwa na muda wowote watapandishwa mahakamani.

Ameongeza kuwa Serikali ina nia njema ya kujenga mazingira wezeshi ya kuweza kutumia mitandao ya mawasiliano na katiba ya nchi inaruhusu wananchi kukosoa kwa lugha ya staha, huku akisisitiza kuwa lugha za matusi, kashfa na kejeli hazitovumilika.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *