NDUGULILE: TPC ANGALIENI UPYA MUUNDO NA SERA YA POSTA

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (katikati) akizungumza katika kikao kazi cha Menejimenti na Mameneja wa Mikoa wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) jijini Dodoma. Kulia ni Waziri wake Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile na Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi.

Na Faraja Mpina – WMTH

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile ameliagiza Shirika la Posta Tanzania (TPC) kuangalia upya muundo wa Shirika hilo pamoja na kurugenzi zake kama vimekaa sawa na kukidhi mahitaji kwa lengo la kuongeza tija, ufanisi na utendaji wa Shirika hilo.

Ad

Dkt. Ndugulile amezungumza hayo alipokuwa akifungua kikao kazi cha Menejimenti na  Mameneja wa Mikoa yote wa Shirika la Posta Tanzania kinachofanyika kwa siku tatu jijini Dodoma ili kujadili utekelezaji wa majukumu ya Shirika hilo katika ngazi ya Mikoa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Zainab Chaula akizungumza katika kikao kazi cha Menejimenti na Mameneja wa Mikoa wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) jijini Dodoma. Kulia ni Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile.

“Mkaangalie upya mgawanyo wa majukumu yenu ili yale yanayoweza kufanyika katika ngazi ya mkoa yafanyike mkoani na yale ya Makao Makuu yafanyikie Makao Makuu, nchi hii ina mikoa 31 jipangeni vizuri kuhakikisha uwepo wa Shirika katika kila Mkoa”, Dkt. Ndugulile

Aidha, amezungumzia Sera ya Posta kuwa ni ya zamani na Sheria yake sio Rafiki sana kuwezesha Shirika hilo kufikia maono yake na maono ya Wizara.

Amesema kuwa Wizara imefanya mabadiliko madogo ya Sheria ya Posta ili kuongeza ufanisi katika utendaji na kusisitiza ni vema kutumia fursa ya kikao kazi hicho kukusanya maoni ya Sera mpya ya posta inayoenda kutengenezwa pamoja na mabadiliko ya sheria yanayotarajiwa.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi akizungumza katika kikao kazi cha Menejimenti na Mameneja wa Mikoa wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) jijini Dodoma, Kulia ni Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile na katikati ni Naibu wake Mhe. Mhandisi Kundo Mathew.

“Shirika ndio mtekelezaji wa Sera ambazo Wizara inaandaa hivyo ni vema Mameneja wakahusishwa ili nao watoe maoni yao pamoja na kuangalia namna ya kujipanga katika utekelezaji wa mipango yao wanayotarajia kuifanya”, Dkt. Ndugulile

Naye Naibu Waziri wake Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amelitaka Shirika hilo kujitangaza zaidi ili kukuza biashara za Shirika hilo  kwa kuanzia ndani ya Shirika kwa kutumia mbinu mbalimbali za kutangaza masoko pamoja na kutengeneza vifaa vyenye nembo ya posta mfano kutengeneza na kutumia shajara zenye nembo ya Shirika hilo.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (wa pili kulia) akizungumza na Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Hassan Mwang’ombe (kulia) baada ya kufungua kikao kazi cha Menejimenti na Mameneja wa Mikoa wa Shirika hilo jijini Dodoma, Katikati ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi akisikiliza na kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew akizungumza jambo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula ametoa angalizo kwa watendaji wa Shirika hilo wanaokaimu nafasi za uongozi kuwa hawatoweza kuthibitishwa katika nafasi wanazokaimu kama hawatofanya kazi vizuri zaidi kwa kujituma ili kuonesha wanastahili kupanda na kuthibitishwa.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Jim Yonazi amewazungumzia watendaji wa Shirika la Posta kuwa ni wasikivu na  wapo tayari kubadilika, kuanzia mameneja mpaka Posta masta Mkuu hivyo ni rahisi kufanya nao kazi kwa sababu wanapokea maelekezo na kuyafanyia kazi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *