Umoja wa Ulaya kupitia Mpango wa Ushirikiano wa 11 chini ya Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya umeipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 111.5 sawa na shilingi bilioni 307.9 kwa ajili ya kufadhili miradi sita ya maendeleo ikiwemo Mradi wa Kuboresha Sekta ya Nishati na Mradi wa kusaidia Kuboresha Mazingira ya Biashara, Ukuaji pamoja na Ubunifu.
Mikataba ya msaada huo ilisainiwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James kwa upande wa Serikali na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Manfredo Fanti.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James aliitaja miradi hiyo kuwa ni Mradi wa Kuboresha Sekta ya Nishati uliopatiwa Euro milioni 35 (shilingi bilioni 96.7) kwa ajili ya kuendeleza sekta ya nishati nchini kwa kuboresha utoaji wa huduma na thamani ya huduma kwa wateja wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Upatikanaji wa nishati safi, mazingira mazuri ya biashara na kuboreshwa kwa sera ya nishati ili kuleta tija na ufanisi pamoja na kuanzishwa kwa kanzidata ya masuala ya nishati kwa ajili ya mipango na maamuzi.
“Mradi wa Matumizi Endelevu ya Nishati ya Kupikia umepewa Euro milioni 30 (shilingi bilioni 82.8) na lengo kuu la mradi huu ni kupunguza madhara yanayosababisha mabadiliko ya tabia nchi hapa nchini kwa kusaidia uzalishaji endelevu wa nishati itokanayo na miti, na kuboresha matumizi bora ya nishati itokanayo na miti sambamba na kuongeza matumizi ya nishati ya kisasa na bora kwa maeneo ya mijini”, alibainisha.
Bw, James alisema Mradi mwingine ni Mradi wa kusaidia Mnyororo wa Thamani katika Ufugaji Nyuki ambao umepatiwa Euro milioni 10 (shilingi bilioni 27.6) kwa ajili ya kuimarisha mchango wa sekta ya ufugaji nyuki katika kukuza uchumi nchi kwa kuhakikisha upatikanaji wa asali yenye ubora inayozalishwa katika mazingira mazuri.
Alisema Mradi wa kuboresha Huduma ya Afya ya Mimea Nchini ili Kuongeza Usalama wa Chakula wenye Euro milioni 10 (shilingi bilioni 27.6) pia ni miongoni mwa miradi hiyo ukiwa na lengo la kuongeza upatikanaji wa mazao salama na bora ya kilimo kwa masoko ya kitaifa na kimataifa.
Aliutaja mradi mwingine kuwa ni Mradi wa Kusaidia Kuboresha Mazingira ya Biashara, Ukuaji na Ubunifu uliopatiwa Euro milioni 23 (shilingi bilioni 63.5) kwa ajili ya kuimarisha Mazingira ya Biashara kwenye mifumo ya leseni, vibali, kanuni na tozo mbalimbali kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara Nchini (Blueprint for Regulatory Reforms).
“Mradi wa Ushirikiano wa Kitaalamu umepewa Euro milioni 3.5 (shilingi bilioni 9.7) kuwezesha Tanzania kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kupitia ushirikiano wa EU na Tanzania. Mradi huu unakusudia kusaidia ukamilishaji wa miradi inayoendelea kutekelezwa kupitia Mpango wa 11 wa EDF; na kusaidia Serikali ya Tanzania katika uandaaji wa miradi mipya itakayofadhiliwa kupitia mpango ujao wa ushirikiano kwa kipindi cha 2021 -2027”, alifafanua Bw. James.
Na. Farida Ramadhani na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Alisema Umoja wa Ulaya ni mmoja wa washirika muhimu katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania na kubainisha kuwa fedha za mikopo na misaada zinazotolewa na umoja huo zimekuwa chachu ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta ya uchumi, uboreshaji wa sera mbalimbali, miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, nishati, kilimo pamoja na mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Naye Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Mhe. Manfredo Fanti alisema msaada huu umelenga kuwanufaisha watanzania na kukuza uchumi wa nchi kwa kuziendeleza sekta muhimu kama nishati na kuweka mazingira mazuri ya biashara nchini pamoja na kuongeza ushindani.
Kwa upande wa Makatibu Wakuu ambao Wizara zao zimenufaika na msaada huo wameushukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada huo na kutoa pongezi zao za dhati kwa Serikali kwa kufanya jitihada mbalimbali za kupata msaada huo utakao chochea maendeleo ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe alisema msaada huo utaipa nchi fursa ya kuhakikisha biashara za ndani na nje zinaongezeka na kukuza ajira na kuongeza makusanyo ya kodi.
Alisema kupitia msaada huo Umoja wa Ulaya umeonesha dhahiri kuwa unaunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki alisema msaada uliotolewa kwa ajili ya Mradi wa Matumizi Endelevu ya Nishati ya Kupikia utasaidia utunzaji wa mazingira kwa kupunguza ukataji miti.
Akizungumzia Mradi wa nyuki ambao pia umepatiwa msaada alisema utatekelezwa katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Shinyanga na Singida kwa Tanzania Bara na kwa Zanzibar utatekelezwa mkoani Pemba.
Tanzania na Umoja wa Ulaya imekuwa na ushirikiano mzuri tangu mwaka 1975 baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya kwanza ya ushirikiano kati ya EU na nchi za Afrika Caribbean na Pacific (ACP) na hadi sasa, Tanzania imepokea kutoka EU takribani Euro milioni 2,394 (sawa shilingi trilioni 6.6) kama misaada, na Euro milioni 270.9 (sawa na shilingi bilioni 748.2) kama mikopo ya masharti nafuu kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB).