Na Jonas Kamaleki, Dodoma
Serikali imetoa shilingi bilioni 49.5 kuimarisha Shirika la Posta na hadi sasa vituo viwili vinavyotoa huduma za pamoja vimeshaanzishwa Dar es Salaam na Dodoma, kwa awamu hii ya kwanza mikoa 10 itafikiwa ikiwemo vituo 2 Pemba na Unguja, Awamu ya pili itafikia vituo (Mikoa) 17 na lengo ni kuwa ifikapo mwaka 2025 mikoa na wilaya zote za Tanzania ziwe na vituo hivi.
Wiki hii Serikali imefanya uzinduzi wa vituo vya huduma za pamoja katika Shirika la Posta. Uzinduzi huu umefanyika Jijini Dar es Salaam na umefanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson msigwa alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari.
“Ningependa kufafanua kidogo kuhusu hizi huduma za pamoja, ni kwamba Serikali imeamua kulifanyia mageuzi makubwa ya kimfumo, kiundeshaji na kiteknolojia Shirika letu Posta ambalo katika miaka ya karibuni lilikuwa hoi biin taabani”, alisema Msigwa.
Moja ya mageuzi hayo makubwa ni kuanzishwa kwa vituo vya huduma pamoja kumwezesha mwananchi kupata huduma mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali katika kituo kimoja. Serikali inataka kupitia vituo hivyo vya huduma pamoja mwananchi akienda pale apate huduma za vitambulisho vya Taifa (NIDA), Huduma za Bima ya Afya, Huduma za Usajili wa Vizazi na Vifo, usajili wa biashara, huduma za kibenki, Huduma za TRA, hifadhi ya jamii na huduma za kusafirisha vifurushi katika kituo kimoja.
Serikali imefanya utafiti na kubaini kuwa kutokana na huduma hizo kutolewa na kila taasisi pekee kivyake, ilikuwa inasababisha usumbufu mkubwa, upotevu mkubwa wa muda na gharama kubwa za watu kufuata huduma. Utafiti umeonesha watu walitumia hadi wiki 4 kupata huduma ambazo sasa zitapatikana katika kituo kimoja kwa muda kati ya dakika chache hadi siku 3.
Aidha, Msigwa amesema kuwa sambamba na hili Serikali inataka Posta iwe shirika linaloendeshwa kisasa. Ukienda kwenye hivi vituo utaona huduma zinatolewa katika madirisha mengi, yaani kila taasisi ina dirisha lake na inatumia mifumo yake. Malengo ya baadaye ni kuwa huduma zile zote zipatikane katika dirisha moja na hiyo itawezekana baada ya mifumo ya kidigitali kuunganishwa.
Lakini huduma zenyewe za Posta zinaboreshwa zaidi ili kwenda kisasa na kidigitali zaidi. Posta hii inakwenda kuwa chombo cha usafirishaji cha kitaifa na kimataifa kama ilivyo vyombo vya mataifa mengine kama DHL, TNT, Royal Cargo n.k, Shirika la Posta linakwenda kuwa Wakala wa mabenki, Bima na taasisi nyingine zinazotoa huduma kwa wananchi, Shirika la Posta tayari limeanzisha Duka Mtandao (www.postashoptz.post) kama ilivyo maduka mtandao ya Alibaba, Amazon, E-bay n.k, na pia Posta inapelekwa kiganjani kwamba sasa Mtanzania na mtu yeyote duniani anaweza kupata huduma za posta kupitia simu ya mkononi. Na Posta ipo kwenye mfumo wa Posta wa Kimataifa na ipo kwa lugha zaidi ya 20.
Ndio Maana unamuona Kaimu Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo anatamba kuwa Posta hii sasa sio Posta ya barua tu, bali ni Posta ya Kidigitali. Tayari Serikali imeshatoa shilingi bilioni 3.9 kwa ajili ya kuiwezesha Posta kuimarisha huduma zake za usafirishaji wa vifurushi vya wananchi, aliongeza Msigwa.
“Fursa za kufanikisha jambo hili zipo, Shirika letu la Posta lina ofisi zaidi ya 300 nchi nzima, ni mwanachama wa Umoja wa Posta Afrika na Duniani. Makao Makuu ya Posta Afrika yapo hapa Tanzania pale jijini Arusha. Lakini pia ni washiriki wa Mkutano wa Mawaziri wa Mawasiliano Duniani (hawa ndio Katibu Mkuu wa Posta Duniani na wanatunga sera za Posta), ni wajumbe wa Baraza la Utawala la Posta Duniani ambalo lina wajumbe 40 (hawa ndio wanasimamia utekelezaji wa Sera na Mikakati kutoka kwa Mawaziri) na ni wajumbe wa Baraza la uendeshaji la Posta Duniani (hili ndilo linaendesha shughuli za kila siku za Posta duniani, na zaidi tunaongoza kamati ya biashara mtandao {e-commerce} ya baraza la uendeshaji)”, alifafanua Msigwa.