- Baraza la Mawaziri limeridhia utozwaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye umeme unaouzwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) na kufuta malimbikizo ya deni la kodi ya VAT lililofikia shilingi Bilioni 22.9 kwa TANESCO kwenye umeme uliouzwa ZECO.
- Baraza la Mawaziri limefanya uamuzi huo leo tarehe 21 Januari, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam, katika kikao kilichoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi na Mawaziri.
- Akizungumza baada ya kikao hicho Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Magufuli amesema baada ya kufanya uamuzi huo Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango atawasilisha marekebisho madogo ya sheria ya VAT, sura ya 148 kupitia sheria ya fedha ya mwaka 2019 ili umeme unaouzwa Tanzania Zanzibar utozwe VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri.
- “Kwa hiyo madeni yatakayokuwa yanadaiwa kwa Zanzibar ni yale madeni ya kulipia umeme, umeme wametumia kiasi fulani wanalipa kama wanavyolipa wa maeneo mengine kwa mfano wanavyolipa Dar es Salaam, suala la kutoza VAT sasa halipo, na katika hilo kwa sababu kulikuwa na deni ambalo lilikuwa limefika shilingi Bilioni 22.9, sisi Baraza la Mawaziri tutapeleka mapendekezo Bungeni kwamba lisamehewe kwa sababu lipo ndani ya bajeti ya mwaka huu wa 2018/19, kwa hivyo litapunguza mapato yatakayotakiwa kukusanywa na Serikali” amesema Mhe. Rais Magufuli.
- Kwa upande wake Mhe. Dkt. Shein amesema pamoja kuridhia utozaji wa VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri, Baraza la Mawaziri pia limekubaliana kuwa Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan ataitisha vikao vya kuzungumzia masuala ya Muungano kila mara kunapokuwa na hoja ya masuala ya Muungano ili kujadili na kutoa uamuzi.
- “Tungependa sana mambo haya yafanyike vizuri kwa sababu pande mbili za Muungano zinatuhusu sote, hili ni muhimu kwa sababu mambo yakikusanyika mengi wananchi wanahisi hatusaidii jitihada zao, kwa hivyo tumeridhia kuwa masuala ya Muungano ambayo yapo chini ya Makamu wa Rais, wakae pamoja wayajadili ili yapate uamuzi wa pande zote mbili” amesema Mhe. Dkt. Shein.
Ad