RAIS MAGUFULI ATOA MSAMAHA KWA WAFUNGWA 4,477

Ndugu Wananchi na Ndugu Watanzania Wenzangu;

Jumapili, tarehe 9 Disemba 2018, nchi yetu (Tanzania Bara), itatimiza miaka 57 tangu kupata Uhuru wake kutoka Utawala wa Uingereza. Napenda, kwanza kabisa, kutumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wazee wetu wote, wakiongozwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kufanikisha kupatikana kwa uhuru wa nchi yetu. Aidha, nawapongeza Watanzania wote kwa kutimiza miaka hii 57 tukiwa wamoja na nchi yetu ikiwa na amani. Hongereni sana Watanzania wenzangu. “Happy Birthday Tanzania Bara”.

Ad

Kama ilivyo ada,  maandalizi ya Sherehe za Uhuru mwaka huu yalikwishaanza.  Takribani shilingi bilioni moja zilitengwa kuadhimisha sherehe hizo. Hata hivyo, kama mlivyosikia kutoka kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nilitoa maelekezo kwamba, mwaka huu tusifanye sherehe. Badala yake, Watanzania wapumzike na kuitumia siku hiyo kutafakari Uhuru tulionao; mahali tulipotoka, mahali tulipo sasa na tunakoelekea. Naomba kusisitiza kuwa tarehe 9 Disemba, 2018 itakuwa Siku ya Mapumziko.

Ndugu Wananchi na Ndugu Watanzania Wenzangu;

Uhuru tulioupata tarehe 9 Disemba, 1961 ulikuwa mwanzo tu wa kuanza harakati za kutafuta uhuru mwingine. Uhuru wa kiuchumi, ambao pengine ni mgumu zaidi kuliko ule wa mwanzo. Napenda kutumia fursa hii kuzipongeza Serikali za Awamu zote za nchi yetu pamoja na Watanzania kwa mafanikio makubwa ya kiuchumi yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 57 iliyopita. Sio siri kuwa Tanzania ya sasa sio sawa na ile ya mwaka 1961. Mambo mengi makubwa yamefanyika nchini mwetu.

Pamoja na ukweli huo, ni wazi kuwa nchi yetu bado ina safari ndefu ya kufika kule tunakotamani kufika; ambako ni kujenga Tanzania iliyo imara zaidi, yenye amani na umoja. Tanzania yenye maendeleo ya kiuchumi na inayojitegemea. Tanzania ambayo huduma za kijamii zinapatikana kwa urahisi zaidi. Tanzania yenye watu walioelimika. Na Tanzania yenye watu wenye kipato kizuri.

Nafarijika kuona kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu tuliyokaa madarakani, Serikali kutekeleza ndoto hiyo. Tumefanikiwa kudumisha Amani, Umoja na Muungano wetu wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Tumeendeleza juhudi za kukuza uchumi. Hivi sasa nchi yetu ni miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakua kwa kasi Barani Afrika. Tumefanikiwa kuwavutia wawekezaji wengi, ambapo mitaji yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 30 imeingia nchini. Tumeimarisha miundombinu mbalimbali na kuboresha huduma nyingine za jamii. Tumepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya rushwa na nchi yetu inatajwa kuwa mfano wa kuigwa. Tumelinda rasilimali zetu.

Wito wangu kwa Watanzania wote, endeleeni kuiunga mkono Serikali yenu. Kama nilivyosema, hivi sasa tupo kwenye vita vya kiuchumi. Vita hii ni ngumu. Hivyo, kila Mtanzania ni lazima ashiriki kwa kutimiza jukumu lake la kuendelea kudumisha amani na umoja, kulinda muungano wetu pamoja na kuchapa kazi kwa bidii. Tuache maneno maneno. Ni lazima tujenge dhana ya kujitegemea katika kujenga Uchumi wetu.

Ndugu Wananchi na Ndugu Watanzania Wenzangu;

Katika kuadhimisha Miaka 57 ya Uhuru, nimeagiza kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya Sherehe zitumike kujenga Hospitali ya Uhuru katika Jiji la Dodoma. Kama mnavyofahamu, ili kutekeleza mawazo ya waasisi wetu, Serikali imeamua kuhamishia rasmi Makao Makuu ya nchi yetu Jijini Dodoma. Hii imefanya mahitaji ya huduma za jamii, ikiwemo afya, kuongezeka. Hivyo, tumeamua kujenga Hospitali nyingine kubwa itakayosaidiana na Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Mkoa.

Sambamba na hayo, katika kuadhimisha Miaka 57 ya Uhuru mwaka huu, nimeamua, kwa mujibu wa Mamlaka niliyopewa kwenye Ibara ya 45 (1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutoa msamaha kwa wafungwa 4,477, ambapo kati yao wafungwa 1,176 watatoka siku ya Maadhimisho ya Uhuru. Msamaha huu utawahusu wafungwa wagonjwa, wazee kuanzia miaka 70 na zaidi, wafungwa wa kike waliongia gerezani wakiwa wajawazito, na waliongia na watoto wanaonyonya au wasionyonya pamoja na wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili.

Halikadhalika, nimeamua kwa wafungwa waliotumikia robo ya adhabu zao, wapunguziwe robo ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa kwenye Kifungu 49 (1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58. Hata hivyo, msamaha huu hautawahusu wafungwa wanaotumikia baadhi ya adhabu, zikiwemo kunyongwa, kifungo cha maisha, biashara ya dawa za kulevya na binadamu, makosa ya unyang’anyi, kukutwa na viungo vya binadamu, makosa ya kupatikana na silaha, risasi, milipuko isivyo halali, makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka, kulawiti, kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekodari, uhujumu uchumi, rushwa, ubadhirifu, ujangili, waliowahi kupunguziwa kifungo kwa msamaha wa Rais, wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole, wenye makosa ya kutoroka au kujaribu ama kusaidia kutoroka chini ya ulinzi halali, waliongia gerezani baada ya tarehe 1 Disemba, 2018 au waliowahi kufungwa na kurudi tena gerezani pamoja na wenye makosa ya kinadhamu magerezani.

Naomba nimalizie salamu zangu kwa kuwatakia tena kila la heri katika Maadhimisho ya Miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

 

Mungu Wabariki Watanzania Wote!

Mungu Ibariki Tanzania!

Mungu Ibariki Afrika!

“Ahsanteni Sana kwa kunisikiliza”

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS DKT. SHEIN AWAAPISHA VIONGOZI ALIOWATEUA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein  amewaapisha viongozi …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *