Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima

Nishati ya umeme itasaidia ukuaji wa uchumi wa viwanda – Naibu Waziri Sima

  • Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima amezitaka nchi zilizoendelea kutimiza wajibu wao wa kutoa michango ya fedha na kuwezesha upatikanaji wa teknolojia za kisasa kwa nchi zinazoendelea kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya Tabianchi kwa mujibu wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na Makubaliano ya Paris.
  • Akihutubia Mkutano wa 24 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaoendeleo Nchini Poland Mhe. Sima ameeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoathirika zaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi duniani, ikiwa ni pamoja na kuathiriwa na ukame, mafuriko na kuongezeka kwa ujazo wa bahari, jambo ambalo huathiri zaidi wakazi wa mwambao wa bahari pamoja na shughuli zao za kiuchumi ambazo ni msingi wa maisha yao.
  • Mhe. Sima amesema kuwa athari hizo zimethibitishwa pia katika taarifa maalumu ya kisayansi iliyotolewa na Jopo la Kimataifa la Wataalamu wa Mabadiliko ya Tabianchi kuhusu athari zitakazojitokeza iwapo joto la dunia litaongezeka zaidi ya nyuzijoto 1.5 (1.50C). “Kwa sasa joto la dunia limeongezeka kwa nyuzijoto 0.85 kulinganisha na kipindi kabla ya mapinduzi ya viwanda, natoa rai kwa jumuia ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na za makusudi kukabiliana na changamoto hii” Sima alisisitiza.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima akihutubia katika Mkutano wa 24 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea Katowice Poland. Pamoja na mambo mengi Mhe. Sima amezitaka Nchi zilizoendelea kutimiza wajibu wao wa kutoa michango ya fedha ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi kwa nchi zinazoendelea.
  • Katika Hotuba yake Naibu Waziri ameeleza juhudi za Tanzania katika kukabiliana na changamoto hizi ambazo zinaendana na mpango wa maendeleo wa Taifa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Mfumo wa usafiri wa mwendo kasi katika jiji la Dar es Salaam, ujenzi wa barabara za juu (flyovers and interchange) na ujenzi wa bwawa la umeme wa maji katika mto Rufiji ambao unatarajiwa kuzalisha umeme kiasi cha MW 2,115.
  • Mhe. Sima amesema kuwa nishati ya umeme ambayo ni salama kimazingira itasaidia katika ukuaji wa uchumi wa viwanda, undeshaji wa treni za umeme na kurahisisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa matumizi ya majumbani na kusisitiza kuwa kuwa hizi ni hatua muhimu katika kusaidia kupunguza uzalishaji wa gesijoto zinazochangia ongezeko la joto duniani.
  • Mhe. Mussa Sima yuko nchini Poland akiongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu ulioanza tangu tarehe 2 Desemba 2018 na unamalizika tarehe 14 Desemba, 2018.
Ad

Unaweza kuangalia pia

WAZIRI ZUNGU AHUDHURIA MKUTANO WA 7 WA BARAZA LA KISEKTA LA MAWAZIRI WA MAZINGIRA NA MALIASILI WA JUMUIA YA AFRIKA MASHARIKI

             

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *