Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Mhandisi James Kilaba akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mwita Waitara (wa pili kushoto) kuhusu kituo cha telesenta wakati wa ziara yao wilayani Sengerema. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Emmanuel Kipole.

WAITARA AZITAKA HALMASHAURI ZOTE KUTEKELEZA MPANGO WA ANWANI ZA MAKAZI NA POSTIKODI NCHI NZIMA

 • Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mwita Waitara amezitaka Halmashauri zote kutekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi nchi nzima kwenye Halmashauri zao bila ya kutumia kisingizio cha ukosefu wa bajeti za kufanya vikao vinavyohusu utoaji wa majina ya mitaa
 • “Suala la gharama halipo, tumieni vikao vyenu vya kawaida, vya kisheria kutaja majina ya mitaa, suala la anwani za makazi na postikodi iwe ajenda mahususi ya ulinzi na usalama”, amefafanua Waitara
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) akijadiliana jambo na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mwita Waitara wakiwa wanatoka kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Sengerema (hayupo pichani) wakati wa ziara yao wilayani humo ya utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi
 • “Wakurugenzi wote wa Halmashauri zote nchi nzima waliopo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI wahakikishe kwamba wanatoa maelekezo mahususi kwa watendaji wote na kuhakikisha kuwa wanatoa majina ya mitaa,” amesema Waitara. Pia amewaelekeza Makatibu Tawala wote Tanzania Bara wahakikishe Halmashauri zote zinatekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi
 • Waitara ameongeza kuwa mpango huu unatuwezesha kujitambua na kuwatambua watu wetu wanakoishi, na nini kilichowaleta eneo hilo kama ni biashara, uwekezaji na ni muhimu kwa ulinzi na usalama wa raia. Pia amesema kuwa suala la anwani za makazi na postikodi litawasaidia viongozi wao wenyewe kuwatambua wananchi, kuwezesha ukusanyaji wa kodi na kufikisha huduma za Serikali kwa wananchi
NAIBU WAZIRI WAITARA
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mwita Waitara akizungumza na viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Sengerema na Buchosa (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi wakiwa Nyehunge, Mwanza. Wa tatu kushoto ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye, wa tatu kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi na wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole
 • “Rais Dkt. JohnMagufuli anataka watanzania walipe kodi, jambo hili likitekelezwa, watanzania watalipa kodi na mpango huu wa kuwatambua wananchi utasaidia kuongeza mapato ambayo yataleta maendeleo ya taifa letu na kujenga miundombinu ya barabara, huduma za afya na elimu,” amesema Waitara
 • “Wenzetu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa upande wa Sekta ya Mawasiliano wametimiza majukumu yao, wanataka majina ya barabara na mitaa ili waweke namba za nyumba, naomba muwasaidie kutimiza wajibu wao, mtoe majina kwenye vikao vyenu ili Wilaya hii iwe kweli ya mfano,” amesema Waitara
NAIBU WAZIRI
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akifafanua jambo kwa viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Sengerema na Buchosa (hawapo pichani) wakati wa mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi yaliyofanyika Nyehunge, Mwanza. Wa nne kushoto ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mwita Waitara na pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi
 • Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amesema kuwa Sengerema ni moja ya Wilaya chache zilizoteuliwa kuwa ya mfano kutekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi ambapo tunahitaji kila Wilaya Tanzania iwe na mitaa na majina ili tufahamu kila mtanzania anakaa wapi, hii itatusaidia katika masuala ya ulinzi, usalama na uchumi
 • Naye Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole amekiri kuwa Sengerema imepata fursa ya kuwa Wilaya ya mfano na ya mwanzo katika utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi ambapo utekelezaji wa mpango huu kwa wilaya ya Sengerema ambayo iko mpakani itasaidia katika masuala ya ulinzi na usalama, ukusanyaji wa mapato na kodi za Serikali.
WAITARA
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa nne kushoto) akiwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mwita Waitara (wa tatu kushoto) kuhusu kituo cha telesenta wakati wa ziara yao Wilayani humo
 • Mwenyekiti wa Halmashauri ya Buchosa, Joseph Henry Kanyumi akizungumza kwa niaba ya viongozi na watumishi waliohudhuria mafunzo ya mpango huo alisema kuwa wametambua umuhimu wa mpango huo. “Nasi tumenufaika na mafunzo hayo na ifikapo tarehe 15 Januari, 2019 tutakuwa tumekamilisha utoaji wa majina ya mitaa,” alisema Kanyumi
 • Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi alisema kuwa ni muhimu kuweka sheria ndogo ndogo katika Halmashauri ili mpango huu uweze kutekelezwa na kudhibiti ujenzi holela pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili mfumo huu uweze kufanya kazi
 • Mpango wa Anwani za Makazi na Postikodi ulianza kutekelezwa kwa majaribio mwaka 2009 kwenye mikoa minne ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Zanzibar ambapo sasa utekelezaji huo unaendelea kwenye Halmashauri 12 na utafanyika kwenye Halamshauri zote nchi nzima. Aidha, hadi sasa kata zote nchi nzima zina postikodi ambazo zimeridhiwa na Umoja wa Posta Duniani (UPU) ambapo tangazo la Serikali Na. 220 lilitolewa kwa mara ya kwanza tarehe 22 Juni mwaka 2012 na kuboreshwa na kutolewa tena tangazo la Serikali Na. 140 tarehe 22 Aprili mwaka 2016. Vile vile, Serikali imeandaa mwongozo wa postikodi na anwani za makazi ili watendaji wa Halmashauri waweze kuzingatia na kutumia kufanikisha utekelezaji wa mpango huu
Ad

Unaweza kuangalia pia

SERIKALI INATARAJIA KUJENGA MINARA 5 YA MAWASILIANO WILAYANI MAFIA

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mh. Injinia Atashasta Nditiye (Mb.) amezindua mnara wa Mawasiliano …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *