WAZIRI KAMWELWE AZINDUA BODI MPYA YA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

 • Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amezindua Bodi mpya ya Shirika la Posta Tanzania (TPC). Uzinduzi huo umefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa jengo la Makao Makuu ya Bandari, Dar es Salaam
 • Wakati akizundua bodi hiyo, kamwelwe amesema kuwa ana imani na bodi hiyo kwa kuwa itaimarisha usimamizi katika utekelezaji wa mikakati mbali mbali ili kuboresha utendaji wa TPC na hivyo kuliwezesha kuchangia katika maendeleo ya taifa letu.
1-01
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Bodi (hawapo pichani) ya Shirika la Posta Tanzania wakati akizindua bodi hiyo, Dar es Salaam
 • Ameongeza kuwa uzinduzi wa bodi hiyo umefuata baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John  Magufuli kumteua Kanali Mstaafu, Dkt. Haruni Kondo kuendelea kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo kwa awamu ya pili baada ya kipindi cha awali kumaliza.
 • “Hii inaonesha imani aliyonayo Mhe. Rais kwako na kuthamini utendaji ulioonesha kwa kipindi kilichopita kwa kusimamia utendaji wa Shirika, Shirika liliboresha utendaji kutoka hati chafu za ukaguzi wa hesabu hadi kufikia kutoa gawio kwa miaka miwili mfululizo. Nina imani utaendeleza utendaji huu mahiri,” amesema Mhandisi Kamwelwe
3-01
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Mawasiliano), Kitolina Kippa akiwatambulisha wajumbe wapya wa bodi ya Shirika la Posta Tanzania kwa Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Isack Kamwelwe (aliyekaa mbele meza kuu), Dar es Salaam
 • Kamwelwe ameitaka Bodi itekeleze majukumu yake ya kuishauri Serikali na kusimamia utendaji kazi wa TPC kwa kuwa ni shirika la umma ambalo linahitajika kuendelea kuwepo ili lihudumie wananchi kwa kusafirisha vifurushi na vipeto na kutoa huduma kwa gharama nafuu kama inavyofanya sasa na liende mbali zaidi kwa kutoa huduma zake kidijitali
 • Vile vile ameiagiza bodi hiyo kuwianisha sheria zinazosimamia utendaji na masuala ya ajira katika shirika hilo kuliko hali iliyo sasa ambapo masuala ya ajira yanashughulikiwa na sheria mbili ambazo ni Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya mwaka 2004 na Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 ambazo zote zinatumika kwa pamoja ambapo katika kipindi kilichopita cha uendeshaji wa shirika, sheria hizi zimeleta migongano kati ya bodi na menejimenti ya shirika
4-01
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania, Kanali Mstaafu, Dkt. Haruni Kondo akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (hayupo pichani) baada ya kuzindua bodi hiyo, Dar es Salaam. Kushoto ni Posta Masta Mkuu wa Shirika hilo, Hassan Mwang’ombe
 • “Ni matumaini yangu kuwa wajumbe wapya wa bodi kama ndugu Erick Shitindi na wengine, mtasaidia shirika kuboresha utendaji wake kwani mna uzoefu wa muda mrefu katika masuala ya uendeshaji wa shughuli mbali mbali za Serikali hususani katika masuala ya miundo, usimamizi wa rasilimali watu na ajira”, amefafanua Kamwelwe
 • Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Mawasiliano), Kitolina Kippa aliwatambulisha wajumbe wa bodi hiyo kwa Mhandisi Kamwelwe ambao ni Dkt. Ubena Agatho John, Bi. Fatma Bakari Juma, Mhandisi Augustine Matthew Mbalamwezi, Erick Francis Shitindi, Bwire Magere na Michael Masinda ambao uteuzi wao ni wa kipindi cha miaka mitatu kuanzia tarehe 20 Januari, 2020.
5-01
Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe akisoma taarifa ya utekelezaji wa majukumu wa Shirika hilo mbele ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (aliyekaa mbele) baada ya kuzindua bodi hiyo, Dar es Salaam
 • Kippa amesema kuwa uteuzi huo ni kwa mujibu wa Sheria iliyoanzisha TPC Na. 19 ya mwaka 1993 pamoja na marekebisho yake yaliyotangazwa kwenye gazeti la Serikali la tarehe 15 Novemba, 2019 kwa tangazo Na. 845/2019
 • Naye Mwenyekiti wa bodi hiyo, Kanali Mstaafu, Dkt. Haruni Kondo amesema kuwa wapo tayari kuendesha TPC kwa spidi ya Mhe.Rais wetu kwa kuwa bodi ina wajumbe wazalendo, TPC imetengeneza faida na shirika liko vizuri, lina uwezo mkubwa na wako tayari kufanya kazi zaidi ili kuongeza faida, kusimamia rasilimali za shirika kwa maendeleo ya taifa letu
 • Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe akisoma taarifa ya utekelezaji wa shirika hilo amesema kuwa shirika linatumia shilingi milioni 69 hadi 75 kwa mwezi kulipa pensheni kwa wastaafu wa iliyokuwa Shirika la Posta na Simu la iliyokuwa  Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo wao sio mfuko wa hifadhi ya jamii
 • Mwang’ombe ameiomba bodi mpya kwa kushirikiana na Serikali iisaidie TPC na kuwawezesha kupata mtaji wa kuendesha shirika hilo kwa faida zaidi ili waweze kuendelea kutoa gawio. Na Prisca Ulomi – WUUM, DSM
Ad

Unaweza kuangalia pia

SERIKALI KUPELEKA MAWASILIANO YA SIMU SINGIDA MASHARIKI

Serikali imeahidi kujenga mnara wa simu katika Kijiji cha Msule kilichopo kata ya Misugha jimbo …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *