SHILINGI BIL. 222 ZIMELIPWA KWA WAKULIMA WA KOROSHO – WAZIRI MKUU MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema jumla ya shilingi bilioni 222 zimelipwa na Serikali kwa wakulima wa zao la korosho na kuwataka wakulima wawe na subira.

Amesema wakulima walioanza kulipwa ni wale wenye kilo zisizozidi kilo 1,500 na wale wenye kilo zaidi ya 1,500 na kuendelea Serikali inaendelea na uhakiki kisha watalipwa.”Fedha zipo, hakuna mkulima ambaye atapoteza haki yake wote watalipwa. Tunaendelea na uhakiki kwa wale wenye korosho nyingi ili kubaini kama hawajanunua kangomba.”

Ad

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Desemba 30, 2018) alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Nandagala ‘A’ baada ya kufungua ofisi ya CCM kata ya Nandagala.Amesema baadhi ya watu wamekutwa na kilo zaidi ya 1,500 na wameshindwa kuonesha mashamba yao ya mikorosho, hali inayodhihirisha kwamba amenunua kupitia kangomba.

Waziri Mkuu amesema baadhi ya waliokutwa na korosho nyingi ni vijana wadogo ambao hawana hata uwezo kifedha hivyo Serikali itahakikisha inawakamata watu wanaowatuma.Amesema lengo la Serikali inayoongizwa na Rais Dkt. John Magufuli ni kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo chao, hivyo biashara ya kangomba lazima lidhibitiwe.Waziri Mkuu ambaye leo ameanza ziara yake kwa kikazi wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi amesema zoezi la ulipaji kwa wakulima wa korosho linaendelea, wakulima wawe na subira.

Serikali iliamua kununua korosho zote za mwaka huu baada ya kubaini wafanyabiashara wamepanga kuwadhulumu wakulima kwa kupanga kununua kwa bei ndogo.Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametembelea eneo la ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Matambalale wilayani Ruangwa ambapo amewataka wahakikishe ujenzi unakamilika.

Amewataka wananchi wa kata hiyo kushirikiana na kuhakikisha wanachangia nguvu kazi katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ili mwakani wanafunzi waanze kusoma.Tunataka tuondoe dhiki ya watoto wetu kutembea umbali mrefu hadi Namichiga kutafuta elimu, tunataka watoto wetu wote wasome katika maeneo yaliyo karibu na makazi yao.”

Amesema wanafunzi zaidi ya 200 wamefaulu na hawana pa kwenda hivyo ni lazima ujenzi wa shule zote za sekondari za Matambalale, Chibura na Ruchelegwa ukamilike.Waziri Mkuu amesema hadi Januari 10, 2019 shule hizo zote lazima ujenzi wake ukamilike ili wanafunzi waanze kusoma, hivyo viongozi washirikiane na wananchi kukamilisha ujenzi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,JUMAPILI, DESEMBA30, 2018.

Ad

Unaweza kuangalia pia

WAZIRI MKUU AKIWA NA WABUNGE MBALIMBALI BUNGENI MJINI DODOMA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *