Baadhi ya nguzo za umeme za zege zenye urefu wa mita 14 ambazo zinatumika katika eneo la mradi umeme wa Rufiji ili kutoathiri maisha ya wanyama katika mbuga ya Selou ambao huweza kuruka kwa urefu wa mita 12.

UJENZI WA MRADI WA UMEME RUFUJI KUANZA RASMI MWENZI JUNI

 • Imeelezwa kuwa ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji utakaozalisha  megawati 2115 unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 15 mwezi Juni mwaka huu.
 • Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani katika eneo utakapotekelezwa mradi huo wilayani Rufiji mkoani Pwani mara baada ya kukagua  kazi za ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi huo ikiwemo barabara, umeme, maji na reli.
Miundombinu ya reli
Miundombinu ya reli katika Kituo cha Fuga wilayani Rufiji mkoani Pwani ambayo inaboreshwa ili kuweza kutumika kushusha mizigo wakati wa utekelezaji wa mradi wa umeme wa Rufiji.
 • Katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati aliambatana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constatine Kanyasu na Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa.
 • Viongozi wengine walioshiriki ziara hiyo ni makatibu wakuu kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Mifugo na uvuvi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
 • Dkt. Kalemani alisema kuwa,  mkandarasi  ambaye ni Arab contractors amepewa miezi 36 ya ujenzi wa mradi huo na miezi sita ya maandalizi hivyo inatarajiwa kuwa mradi utakamilika mwezi Aprili  mwaka 2022.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa Tano kushoto) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (wa pili kulia) wakiangalia kazi ya urekebishaji wa miundombinu ya barabara katika eneo kutakapojengwa mradi wa umeme wa Rufiji. Wengine katika picha ni viongozi kutoka Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali zinazohusika na utekelezaji wa mradi huo.
 • Kuhusu ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi, Dkt Kalemani alisema kuwa kazi za ujenzi wa miundombinu hiyo iliyoanza miezi tisa iliyopita imekamilika kwa zaidi ya asilimia 80 .
 • Aliongeza kuwa, ili kutekeleza mradi huo, jumla ya megawati 30 zitahitajika katika eneo hilo ambapo mpaka sasa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeshafikisha megawati 10 huku  mahitaji ya umeme kwa sasa yakiwa ni megawati 7.
 • Hivyo,  aliiagiza  TANESCO kuendelea kuratibu kazi hiyo ili nishati hiyo isiwe kikwazo cha kuchelewesha utekelezaji wa mradi.
 • Aidha pamoja na kuzipongeza  taasisi zote zinazohusika na mradi huo,  alitoa wito wa kuendelea kushirikiana ili kukamilisha kazi ndani ya wakati na kwa ufanisi kwani mradi huo ni wa Serikali.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa kwanza kushoto) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (wa pili kushoto) wakiwa katika eneo kunapojengwa nyumba zitakazotumiwa na mkandarasi atakayejenga mradi wa umeme wa Rufiji zilizopo katika eneo hilo la mradi.
 • Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliwapongeza TANESCO kwa kutekeleza kazi zao kwa ufanisi katika eneo hilo la mradi na  viongozi wa wizara ya nishati kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
 • Alisema kuwa,  Wizara hiyo ilipewa kazi mbalimbali ikiwemo kupima eneo lote la mradi na kueleza kuwa wameshamaliza kupima maeneo mawili ya mradi huo ambapo eneo la kwanza ni litakalojengwa mitambo ya umeme lenye hekta 1402 ambalo mchoro wake umekamilika.
 • Pia, Wizara hiyo  imepima eneo lenye hekta 4711 litakalojengwa nyumba za kudumu za wafanyakazi na kwamba wameshaweka alama katika maeneo hayo ambapo alimkabidhi Waziri wa Nishati michoro ya maeneo hayo ili taratibu nyingine za umiliki ziendelee.
 • kwa upande wake,  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  alisema kuwa,  Wizara yake inaendelea majukumu mbalimbali yatakayowezesha kuanza kwa mradi huo ikiwemo usafishaji wa sehemu itakayokuwa ni bwawa la kuhifadhia maji ya kuzalishia umeme.
 • Aliongeza kuwa,  kazi hiyo wameigawa katika  blocks 30 na kwamba blocks 27 zimeshapata watu wa kufanya kazi hiyo na baadhi ya waombaji tayari wanaendelea na kazi husika.
 • Kuhusu ulinzi alisema kuwa, wanatoa ulinzi katika eneo hilo na kwa watu wote wanaofanya kazi za mradi na kwamba awali kulikuwa  na askari 115 lakini wameongeza askari wengine 115 ili kukidhi mahitaji na kueleza kuwa idadi hiyo itaongezeka kadri kazi zinavyoongezeka.
 • Viongozi waliohudhuria ziara hiyo kutoka Wizara ya Nishati, ni Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia maendeleo ya nishati, Mhandisi Juma Mkobya na Kaimu Mkurugenzi Msadizi wa Ufuatiliaji na Tathmini, Lusajo Mwakaliku.

 

Ad

Unaweza kuangalia pia

WAZIRI KALEMANI AFUNGUA KIWANDA CHA NGUZO ZA UMEME – KIGOMA

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, amefungua kiwanda cha Nguzo cha Qwihaya, kilichopo katika Mtaa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *