- Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imesema katika kipindi Cha Miaka mitatu imeweza kufanya mambo mbalimbali ya udhibiti wa usalama, ubora na usalama wa bidhaa za ndani na nje ya Nchi ikiwemo kutambulika kimataifa kwa kuzingatia viwango vya Kimataifa vya ISO 9001: 2015.
- Hii ni kutokana na mafanikio ya miaka mitatu ya utekelezaji wa kazi chini ya Serikali ya Awamu ya Tano, kwa kufikia na kuvuka malengo iliyojiwekea katika udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi ili kulinda afya ya jamii nchini.
- Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Bw. Adam Fimbo amebainisha hayo wakati akitoa ripoti ya miaka mitatu ya Mamlaka hiyo wakati wa ziara maalum ya Maafisa Mawasiliano na habari wa Wizara ya Afya na taasisi zake katika kampeni maalum ya ‘Tumeboresha Sekta ya Afya’ inayolenga kueleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.
- “Kutokana na kuwa na mifumo thabiti ya udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa, mnamo Mwezi Desemba 2018, TFDA imetambulika kufikia ngazi ya tatu (Maturity Level 3) ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya ubora wa mfumo wa udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vipodozi, ambapo hatua hii imeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia hatua hii
- Fimbo ameeleza kuwa, TFDA katika mikakati yake hiyo imeweka mifumo na taratibu za ndani za utoaji huduma na utendaji bora ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya ISO 9001:2015 kwa huduma za kawaida na ISO 17025:2005 kwa huduma za maabara.
- Aidha, ameongeza kuwa huduma za TFDA hutolewa kwa kuzingatia viwango vya Mkataba wa Huduma Wateja kama ulivyorejewa mwaka 2016.
- “Mfumo wa usajili wa bidhaa umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka ambapo idadi ya bidhaa za chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi vilizosajiliwa imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, katika kipindi cha 2015/16 hadi 2017/18.
- Pia tumesajili jumla ya bidhaa 14,345 kutoka bidhaa 8,866 zilizokuwa zimesajiliwa mwaka 2015/16 ambapo ni sawa na ongezeko la 62%. Hii imetokana na kuongezeka kwa uelewa wa matakwa ya sheria miongoni mwa wafanyabiashara na kukua kwa biashara.” Ameeleza Fimbo.
- Aidha, Fimbo ameongeza kuwa TFDA imekuwa ikifanya tathmini na usajili wa bidhaa kwa lengo la kuhakiki endapo bidhaa zinakidhi vigezo vya usalama, ubora na ufanisi kabla ya kuruhusiwa katika soko.
Ad