- Serikali imesema kuwa kwa sasa nchi haina tatizo la mzunguko mdogo wa fedha katika soko kutokana na hatua mbalimbali ilizozichukua kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuongeza ukwasi kwenye uchumi.
- Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Momba Mhe. David Silinde (Chadema), aliyetaka kujua sababu za mzunguko mdogo wa fedha.
- Dkt. Kijaji alisema kuwa, katika kutatua changamoto ya kupungua kwa mzunguko wa fedha katika soko, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilichukua hatua mbalimbali za kuongeza ukwasi kwenye uchumi ikiwemo kushusha riba ya Benki Kuu (discount rate) kutoka asilimia 16 kwa mwezi Machi, 2017 hadi asilimia 7, Agosti 2018.
- “Benki Kuu ilipunguza kiwango cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na mabenki ya biashara(Statutory Minimum Reserve Requirement, (SMR)) kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8 mwezi April 2017 pamoja na kuruhusu mabenki kutumia asilimia 10.0 ya sehemu ya SMR kama chanzo kimojawapo cha kusaidia hali ya ukwasi kwenye uchumi”, alisema Dkt. Kijaji.
- Alisema Benki Kuu ilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo ya muda maalumu kwa mabenki pamoja na kununua fedha za kigeni kutoka kwenye soko la jumla la mabenki ili kuongeza ukwasi kwenye uchumi.
- Alifafanua kuwa mzunguko wa fedha katika uchumi unaendana na malengo pamoja na mahitaji halisi ya shughuli za kiuchumi zizopo kwa sasa.
- Aidha, Dkt. Kijaji alisema Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania inatekeleza Sera ya Fedha inayolenga kusimamia mzunguko wa fedha unaoendana na mahitaji halisi ya uchumi kwa lengo la kudumisha utulivu wa mfumuko wa bei na hivyo kuweka mazingira mazuri ya ukuaji wa uchumi.
Ad