UHAMASISHAJI WA UTAFITI UTAWEZESHA UHIFADHI NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA

  • Tathimini za uwekezaji katika kutunza mazingira katika nchi ni moja ya kazi muhimu za Ofisi ya tathmini ya Baraza la Kituo cha Kimazingira Duniani (GEF) linalotoa taarifa na matokeo ya jumla ya miradi na utendaji katika ngazi ya kitaifa.
  • Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA) ambao ni mwongozo muhimu katika kuleta maendeleo endelevu, unatambua kuwa mazingira bora ni msingi wa maendeleo endelevu na kupunguza umaskini.
  • Mkakati huu umeainisha malengo 15 yanayohusu mazingira na utekelezaji wa MKUKUTA unahusisha wadau mbalimbali, ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais (OMR) inalo jukumu la kuratibu ujumuishaji wa masuala ya mazingira katika mipango na bajeti za kisekta za kupunguza umaskini.
  • Katika kutekeleza jukumu hili, OMR imefanikisha na inaendelea kutekeleza mipango na programu kadhaa ikiwemo ile ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira, Sheria ya Mazingira na Kanuni zake.
  • Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 imeeleza wazi wajibu na majukumu ya wadau mbalimbali kuanzia serikali za mitaa hadi taifa ikisisitiza mipango na usimamizi wa matumizi endelevu ya mazingira: kudhibiti uchafuzi wa mazingira; utunzaji wa taarifa na takwimu za mazingira; utafiti na ushiriki wa jamii na utekelezaji wa majukumu yatokanayo na mikataba ya kimataifa.
  • Akiwasilisha Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Nchi Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba anasema Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kutekeleza Ajenda ya Taifa ya Utafiti katika Mazingira (NERA 2017-2022).
  • Waziri Makamba anasema katika mwaka wa fedha 2017/18, NEMC kwa kushirikiana na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kamisheni ya Matumizi ya Ardhi, Taasisi ya Huduma za Misitu na Halmashauri ya Wilaya ya Same imefanya tathmini ya hali ya mazingira kwenye maporomoko  ya ardhi katika milima ya Mamba Miamba iliyopo Wilayani Same.
  • Anaongeza kuwa katika tathmini ya utafiti huo ilibaini chanzo cha maporomoko hayo ni aina ya udongo wa mfinyanzi uliopo katika eneo hilo pamoja na shughuli za kibinadamu zinazofanyika huko ikiwa ni pamoja na ukataji holela wa miti na uchomaji moto hovyo katika maeneo hayo.
  • Aidha anasema NEMC limepeleka mapendekezo ya kuzuia uharibifu wa mazingira katika eneo hili kwa wadau ili hatua thabiti za uhifadhi zichukuliwe, ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kulitangaza eneo hilo kuwa ni eneo tete la mazingira na kulitengenezea mpango wa kudhibiti uharibifu wa mazingira.
  • “Katika mwaka 2017/18, Baraza limefanya utafiti wa uharibifu wa  mazingira wa Bwawa la Mindu lililopo katika Manispaa ya Morogoro na mmonyonyoko wa ardhi  katika  fukwe za Ziwa Viktoria. Matokeo ya tafiti hizo yalibainisha vyanzo mbalimbali vya uharibifu na kupendekeza hatua za kuchukuliwa” anasema Waziri Makamba.
  • Kwa mujibu wa Waziri Makamba anasema NEMC imefanya utafiti wa namna ya kuboresha mazingira ya mji wa Dodoma ili uwe ‘mji wa kijani’ kwa kutumia dhana  za  green city, eco-buildings na sustainable construction.
  • Akifafanua zaidi anasema katika mwaka 2017/18, Baraza limeendelea kuratibu shughuli za Hifadhi Hai kwa kuwasilisha taarifa za awali katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa ajili ya kuingiza Hifadhi ya Gombe Ugalla -Masito kwenye mtandao wa Hifadhi Hai za Dunia.
  • Waziri Makamba anasema NEMC pia imeandaa Mpango wa Usimamizi wa Mazingira (Environmental Management Plan-EMP) kwa maeneo mawili ambayo ni Dakio la Bonde la Kihansi na eneo la Ziwa Chala–Jipe. Aidha, Baraza limekamilisha zoezi la uwekaji mipaka katika eneo la Kihansi ambalo linatarajiwa kutangazwa kuwa eneo lindwa la kimazingira.
  • Anasema katika mwaka 2018/19, Baraza litaendelea kukusanya takwimu na na kuandaa taarifa za hali ya mazingira ya milima nchini, taarifa ya mazingira ya pwani (State of the Coastal Environment Report – SOCR, 2018); utafiti wa mifumo ya ikolojia ya hali ya mabonde ya mito mikubwa, maeneo ya malisho ya mifugo na wanyamapori.
  • Tanzania ni nchi yenye uwezo mkubwa wa kuweza kutoa manufaa kimazingira duniani, kwa kuzingatia changamoto za kimazingira za kitaifa na kimataifa zinazoikumba nchi ni wajibu wa wadau wa kitaifa na kimataifa kuwekeza rasilimali ili kukuza, kuchangia na kuthibiti maliasili ili kuboresha na kuongeza mchango wa Tanzania katika mazingira Duniani.
Ad

Unaweza kuangalia pia

WAZIRI ZUNGU AHUDHURIA MKUTANO WA 7 WA BARAZA LA KISEKTA LA MAWAZIRI WA MAZINGIRA NA MALIASILI WA JUMUIA YA AFRIKA MASHARIKI

             

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *