Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye (wa 4 kutoka kulia) akikagua mbao za Gati la Kilindoni Wilayani Mafia.

TATIZO LA USIKIVU WA MAWASILIANO MAFIA KUKAMILIKA NDANI YA MIEZI 7

  • Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye (Mb.) amewaahidi wakazi wa Kisiwa cha Mafia kuwa Serikali imejipanga kuboresha mawasiliano katika vijiji vitatu vyenye usikivu hafifu wa mawasiliano ya simu za mkononi.
  • Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Miburani, Chunguruma na Banja kisiwani Mafia wakati wa ziara ya kukagua usikivu wa mawasiliano ya simu za mkononi, alisema anatambua na amethibitisha kuwa wananchi wa vijiji hivyo wanapata usikivu hafifu na kuahidi kuwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Serikali itaboresha mawasiliano hayo katika kipindi cha miezi saba kuanzia mwezi huu wa Aprili.
NAIBU KATIBU MKUU
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Jim Yonazi akisalimia wananchi wa Mafia wakati wa mkutano wa Naibu Waziri Uchukuzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye kusikiliza kero za wananchi wa Wilaya hiyo kuhusu masuala ya usafiri na mawasiliano.
  • Nditiye amesema hayo katika ziara ya kukagua usikivu wa mawasiliano na masuala ya Uchukuzi akiwa ameongozana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwenye dhamana ya Sekta ya Mawasiliano Dkt. Jim Yonazi, Mbunge wa Mafia Mbaraka Dau (Mb.) pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Injinia Peter Ulanga.
  • “Nawaomba muwe na subira, serikali inalitambua hili na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote utahakikisha kuwa mawasiliano yanakuwa bora na yenye usikivu wa kutosha,” aliahidi Nditiye.
  • Pamoja na kukagua usikivu wa Mawasiliano katika kisiwa cha Mafia, Nditiye pia alikagua uwanja wa ndege wa Mafia na kumuagiza Meneja wa Uwanja huo kupeleka mara moja makao makuu mahitaji ya kuboresha uwanja huo ili kuhakikisha unafanya kazi kwa viwango vinavyohitajika kwa ajili ya usalama wa usafiri wa anga kisiwani humo.
  • Vilevile Nditiye alifanya ukaguzi katika gati ya Kilindoni na kuagiza matengenezo ya mbao za gati hiyo zifanyiwe ukarabati na matengenezo mengine muhimu mara moja kuanzia wiki hii na taarifa za kukamilika kwa marekebisho hayo zipelekwe Wizarani mara matengenezo yatakapokamilika.
  • Pia  Nditiye alizungumza nawananchi wa Mafia na kupokea kero za wananchi kuhusu masuala ya usafiri hususani barabara na vivuko. Akizungumzia suala la kivuko, alisema kivuko kipya kimeanza kutengenezwa na kinategemewa kukamilika hivi karibuni. Hali kadhalika aliwaambia wananchi kuwa wakati kivuko kipya kinatengenezwa, kivuko kilichopo Chuo cha Mabaharia Tanzania kitaanza kuhudumia wananchi katika kipindi cha mwezi mmoja kwa ajili ya usafiri kati ya Jiji la Dar es Salaam, Kilindoni, Mafuya na Nyamisati Kibiti.
  • Nditiye alimshukuru sana Mbunge wa Mafia Dau kwa kuwa mstari wa mbele kusimamia maendeleo ya Mafia katika maeneo yote ya Uchukuzi na Mawasiliano na aliahidi Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na  Rais Dkt. John Pombe Magufuli inafanya kila linalowezekana kuhakikisha maeneo yote ya Tanzania yanafikika kwa usafiri na mawasiliano.
  • Aidha aliwaeleza wananchi wa Mafia kuwa ujenzi wa gati la Nyamisati limefikia asilimia 88 na inatarajiwa litakamilika hivi karibuni na kuondoa kero za wananchi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakipata shida ya usafiri katika Kisiwa cha Mafia.
Ad

Unaweza kuangalia pia

DC CHONGOLO ASITISHA VIBALI VYA UCHIMBAJI MCHANGA MABONDENI KATIKA WILAYA YA KINONDONI

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo amesitisha vibali vya uchimbaji mchanga vilivyotolewa na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *