WAZIRI MKUU ATEMBELEA OFISI MPYA ZA WIZARA YA NISHATI, MTUMBA, DODOMA

  • Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amefanya ziara ya kukagua ofisi mpya za Wizara ya Nishati na Wizara nyingine zilizopo Mtumba jijini Dodoma ili kuona kama lengo la Serikali la kutoa huduma kwa wananchi katika eneo hilo limefanikiwa.
WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (kushoto) akisalimiana na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) wakati alipofika katika Ofisi mpya za Wizara ya Nishati zilizopo Mtumba, jijini Dodoma. Katikati ni Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani.
  • Waziri Mkuu alifanya ziara hiyo tarehe 23 Aprili, 2019 ambapo aliambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ambapo katika Jengo la Wizara ya Nishati, alipokelewa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, na viongozi wengine wa Wizara.
  • “Moja ya lengo letu ni kuwa na eneo moja la kutolea huduma za Serikali kwa wananchi, nimefurahi kuona Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na watoa huduma wote wanaendelea na kazi zao katika eneo hili na huduma zinaendelea kutolewa kwa wananchi.” Alisema Waziri Mkuu.
WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani wakati alipofika katika Ofisi mpya za Wizara ya Nishati zilizopo Mtumba, jijini Dodoma.
  • Alisema kuwa, atakuwa akifanya ziara za mara kwa mara katika eneo hilo ili kuona mwenendo wa utoaji wa huduma na kusikiliza maoni ya wananchi ili kuweza kufanya marekebisho mbalimbali yatakayopelekea  kuboresha utoaji wa huduma.
  • “Mawaziri hakikisheni kwamba huduma zote zinapatikana hapa na wananchi na wadau mbalimbali wanapata taarifa kuwa huduma zinatolewa katika eneo hili na watumishi waliobaki wanahamia katika Mji huu wa Serikali.” Alisema Waziri Mkuu.
WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (kulia) akizungumza jambo na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) wakati alipofika katika Ofisi mpya za Wizara ya Nishati zilizopo Mtumba, jijini Dodoma.
  • Aliongeza kuwa, Wizara zote zihakikishe zinasimamia masuala mbalimbali ikiwemo upandaji wa miti, kuratibu matumizi mazuri ya ardhi iliyopo, kuwa na vifaa kazi vya kutosha, na kuhakikisha kuwa vikao mbalimbali vinafanyika katika ofisi hizo za Serikali.
  • Aidha, alitoa wito kwa wawekezaji wa ndani na  nje ya nchi  kuwekeza kwenye ujenzi nyumba za gharama za nafuu kwa ajili ya watumishi na kuongeza kuwa, fursa zipo hivyo wakati wowote wanapotaka kujenga waende moja kwa moja kwa Mkurugenzi wa Jiji kwa kuwa ardhi ipo.
  • Vilevile alisema kuwa, yapo masuala yanayoendelea kuboreshwa kama vile maji, barabara na umeme, na katika suala la umeme, alitoa maelekezo kuwa, Wizara ya Nishati ihakikishe kunakuwa na nishati ya umeme ya kutosha itakayowezesha kazi mbalimbali katika eneo hili zinafanyika kwa ufanisi.
WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (kushoto) akiwa kwenye kikao na viongozi wa Wizara ya Nishati mara alipofanya ziara katika Ofisi mpya za Wizara ya Nishati zilizopo Mtumba, Dodoma. Wa kwanza Kushoto kwa Waziri Mkuu ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama na anayefuatia ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.
  • Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani alieleza kuwa, Wizara kupitia TANESCO inaendelea kuboresha hali ya umeme katika eneo hilo na inatarajia kuweka underground cable (nyaza za umeme za ardhini).
  • Alisema kuwa, kazi hiyo inatarajiwa kuanza mwezi wa kwanza mwaka 2020, hii ni baada ya kukamilika kwa kazi ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika eneo hilo ambapo kiasi cha shilingi bilioni 22 kitatumika kwenye mradi huo.
  • Alieleza kuwa, nyaya hizo zina faida mbalimbali ikiwemo upatikaji wa umeme wa uhakika kwani nyaya hazitaathirika na upepo, miti au mvua na pia ni salama zaidi kuliko nyaya zinazopitishwa juu kwenye nguzo.
Ad

Unaweza kuangalia pia

SPIKA WA BUNGE AZINDUA JENGO LA MAHAKAMA WILAYA YA KONDOA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai (Mb) leo azindua …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *