Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi waliohudhuria kwenye uzinduzi wa Maabara ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Aprili 29, 2019.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

WAZIRI MKUU AZINDUA MAABARA YA KISASA YA TUME YA NGUVU ZA ATOMIKI TANZANIA

  • WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka taasisi zinazofanya uhakiki na upimaji bidhaa nchini zijirekebishe na ziongeze kasi ya utoaji matokeo kwa wateja.
  • “Kumekuwa na malalamiko kutoka mipakani juu ya bidhaa zinazochukuliwa ili zikapimwe kwamba zinachukua muda mrefu. Punguzeni urasmi huo ili kufanya sekta ya biashara iweze kwenda kwa haraka zaidi. Tume yako (TAEC), TBS na TFDA ni miongoni mwa taasisi zinazolalamikiwa na wawekezaji na wafanyabiashara. Tumieni fursa hii kujirekebisha na kuharakisha utoaji wa matokeo,” amesema.
PMO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza, katika mkutano wa Pili wa Pamoja wa Mtandao wa Vyombo vya Udhibiti wa Nyuklia kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Aprili 29, 2019.
  • Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Aprili 29, 2019) wakati akizindua maabara ya Maabara ya kisasa ya Teknolojia ya Nyuklia ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (Tanzania Atomic Energy Commission -TAEC) iliyopo Njiro, jijini Arusha.
  • “Nafahamu kuwa hii Tume inafanya kazi kwa karibu na bandari vituo vya mipakani ili kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini. Naamini kuanzia sasa mtaharakisha upimaji wa bidhaa na vifaa na kutoa majibu ya vipimo haraka,” amesema.
PMO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Meneja Muandamizi wa Kituo cha Kimataifa cha Sayansi na Teknolojia na Mshauri wa Masuala ya Kidiplomasia (ISTC), Dkt. Kamen Velichkov, baada ya kufungua mkutano wa Pili wa Pamoja wa Mtandao wa Vyombo vya Udhibiti wa Nyuklia kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Aprili 29, 2019.
  • Waziri Mkuu ameitaka Bodi na Menejimenti ya Tume, waendelee kubuni na kuibua miradi mingine zaidi ya matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia. “Angalieni uwezekano wa kuanzisha kinu cha utafiti kinachotumia teknolojia ya nyuklia (Research Reactor); mtambo wa kuongeza thamani na ubora wa vitu mbalimbali ikiwemo matunda na mazao mbalimbali (multi-purpose irradiator); na mtambo wa kuzalisha dawa za kuchunguza na kutibu maradhi ya saratani (accelerator).”
  • Amesema kwa kufanya hivyo, maabara hiyo na watumishi wake wataongeza mchango wa teknolojia ya nyuklia kwenye ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
PMO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi waliohudhuria kwenye uzinduzi wa Maabara ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Aprili 29, 2019.
  • Amesema anatambua kwamba Tume ya Nyuklia Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa wafanyakazi na ufinyu wa bajeti ya ujenzi wa maabara awamu ya pili. “Serikali inazichukua changamoto hizo na itaendelea na juhudi za kuzitafutia ufumbuzi kadiri hali ya kiuchumi itakavyoruhusu,” amesema.
  • Waziri Mkuu ameishukuru Jumuiya ya Ulaya kwa msaada wa vifaa vya maabara hiyo vyenye thamani ya Euro milioni 2.2 (sawa na sh. bilioni 7.5) na kwamba Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano katika sekta mbalimbali.
PMO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikata utepe wakati alipozindua Maabara ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Aprili 29, 2019.
  • Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameiagiza Bodi na uongozi wa Tume hiyo wawapandishe vyeo watumishi watatu wa tume hiyo ambao aliwapa vyeti na zawadi ya sh. milioni moja kila mmoja kwa kukataa rushwa na kutokubali vitisho walivyopewa.
  • “Nimefurahi sana kuona watumishi watatu ambao ni wazalendo na wamekataa kupokea rushwa au kukubali vitisho walivyokuwa wakipewa na kuamua kusimamia misingi ya kazi zao. Hii zawadi mliyowapa haitoshi.”

PMO

  • “Watumishi hawa ni mfano wa kuigwa na wengine. Mwenyekiti wa Bodi waongeze fedha nyingine kila mmoja sh. milioni mbili ili jumla iwe milioni tatu na wapandishwe vyeo huko waliko ili iwe motisha zaidi kwao. Sijui muundo wenu ukoje, lakini nataka nipate taarifa ya utekelezaji wa haya maamuzi kesho kutwa, baada ya Mei mosi,” amesisitiza.
PMO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akioneshwa kifaa cha kupimia vifaa vya kupimia mionzi na Mkurugenzi wa Kinga ya Mionzi, Dkt Firm Banzi, baada ya kuzindua Maabara ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Aprili 29, 2019.
  • Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu awape vyeti na zawadi, Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Najat Mohamed aliwataja watumishi hao kuwa ni Machibya Matulanya wa kituo cha Mtwara na mpaka wa Kilambo (Tanzania) na Msumbiji; Patrick Simpokolwe na Geofrey Kalolo wa kituo cha Tunduma (Tanzania) na Zambia.
  • Machibya Matulanya ambaye cheo chake ni mtafiti wa mionzi daraja la pili (Radiation Health Physics Research Officer II) amekuwa akitegewa mitego ya rushwa na kupokea vitisho kutoka wa wafanyabiashara na watumishi wa Serikali.
PMO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimkabidhi cheti na pesa kwa kutambua uaminifu wao kwa Mtafiti wa Mionzi Daraja la Pili, Machibya Matulanya baada ya kuzindua Maabara ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Aprili 29, 2019.
  • Patrick Simpokolwe ambaye cheo chake ni mkaguzi wa usalama wa mionzi daraja la pili (Radiation Safety Inspector II) na Geofrey Kalolo ambaye ni mtumishi wa kujitolea (volunteer) naye pia anafanya kazi kama mkaguzi wa usalama wa mionzi daraja la pili. Wote kwa pamoja walipokea vitisho walipozuia mzigo kutoka Zambia wenye thamani ya zaidi ya milioni 20 usiingizwe nchini.

 

Ad

Unaweza kuangalia pia

MATUKIO YA WAZIRI MKUU BUNGENI MJINI DODOMA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *