Rais Dkt. John Pombe Magufuli, amerejea hapa nchini akitokea nchini Zimbabwe ambako amefanya Ziara Rasmi ya siku 3 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.
Kabla ya kufanya ziara nchini Zimbabwe, Mhe. Rais Magufuli amefanya ziara nchini Afrika Kusini ambako pamoja na kuhudhuria sherehe za uapisho wa Rais wa Awamu ya Tano wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amefanya mazungumzo na kiongozi huyo, Ikulu Jijini Pretoria.
Baadaye, Rais Magufuli akaelekea nchini Namibia ambako amefanya Ziara ya Kitaifa kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Dkt. Hage Geingob ambapo pamoja na kufanya nae mazungumzo alifungua mtaa mkubwa uliopatiwa jina la Baba wa Taifa la Tanzania Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na pia alitembelea eneo walipozikwa mashujaa wa ukombozi wa Namibia na kiwanda cha nyama cha Meatco.
Alipowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wakiongozwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Mabeyo.