BEI YA PAMBA NI SH. 1,200 KWA KILO – WAZIRI MKUU

  • Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ana imani kuwa ununuzi wa zao la pamba utaanza mara moja kwa bei ya sh. 1,200 kwa kilo moja katika mikoa yote inayozalisha zao hilo.
  • Amefikia uamuzi huo baada ya kuwepo kwa sintofahamu ya bei kwa takriban ya wiki nne tangu bei elekezi ilipotangazwa Aprili 30, 2019 mkoani Shinyanga kwamba bei hiyo ianze kutumika kuanzia Mei 2, 2019.
PM
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika mkutano wa dharura wa baadhi ya wadau wa zao la pamba aliouiitisha kwenye Ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza, Mei 29, 2019. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela na kushoto ni Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa.
  • Alikuwa akizungumza na wadau wa sekta ndogo ya pamba kwenye kikao kilichofanyika (Jumatano, Mei 29, 2019) kwenye ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu, jijini Mwanza. Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Mawaziri wa Kilimo na Viwanda, Makatibu Wakuu wa Kilimo na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na  Wakuu wa Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu na Geita.
  • Wengine ni wawakilishi wa Wabunge wa mikoa hiyo, Makatibu Tawala wa mikoa, Wakuu wa Wilaya zote za mikoa hiyo, na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya hizo. Pia kilihudhuriwa na wanunuzi wa pamba, wakulima na maafisa wa benki kadhaa.
PM 2-01
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa dharura wa baadhi ya wadau wa zao la pamba wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa wakati alipozungumza katika mkutano aliouitisha kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza, Mei 29, 2019.
  • Waziri Mkuu aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba Serikali bado inaendelea kutafuta njia nzuri ya kuwakutanisha wadau wa mazao ya kibiashara ili yaweze kuwa na tija kwa wakulima. Alisema kazi hiyo inafanywa wa Wizara ya Kilimo. Mazao hayo ni pamba, chai, kahawa, korosho, tumbaku na chikichi.
  • Pia alisema Bodi ya Pamba iachiwe jukumu la kutoa leseni za ununuzi wa zao hilo na kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri waliokuwa wakifanya kazi hiyo waache mara moja. “Kuna baadhi ya Wakurugenzi wanatoa leseni za ununuzi, lakini wenye Mamlaka ni Bodi ya Pamba. Mnunuzi nenda Bodi ukapate leseni yako,” alisema Waziri Mkuu.
PM
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya zinazolima zao la pamba katika mkutano wa dharura wa baadhi ya wadau wa zao la pamba kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza, Mei 29, 2019.
  • Alitumia fursa hiyo kuwakemea baadhi ya wakurugenzi ambao wamekuwa wakizuia wanunuzi wapya kwenye maeneo na kuendelea kuwakumbatia wanaowataka wao. “Wakurugenzi baadhi yenu mnazuia wanunuzi wapya, mnamtaka fulani tu. Kwa kufanya hivyo, unapungua kiwango cha kilo ambacho wakulima wako wangeuza,” alionya.
  • ‘Wanunuzi nendeni mkajitambulishe kwa Wakuu wa Wilaya au Wakurugenzi ili watambue kwamba mpo kwenye maeneo yao lakini kila mnunuzi anayo haki ya kwenda kununua pamba mahali popote hapa nchini.”
  • Kuhusu ubora wa pamba, Waziri Mkuu alitaka wananchi waelimishwe ili waache kuweka maji au mchanga kwenye pamba kwa minajili ya kuongeza uzito kwani kwa kufanya hivyo wanachafua jina la Tanzania pindi inapopelekwa kuuzwa nje ya nchi.
PM
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa dharura wa baadhi ya wadau wa zao la pamba wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa wakati alipozungumza katika mkutano aliouitisha kwenye ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza, Mei 29, 2019.
  • Pia alitaka vyama vikuu vya ushirika vijiridhishe kuhusu ubora wa maghala ya kuhifadhia pamba kwenye vyama vya msingi (AMCOS) kwani kwa kufanya hivyo, itawasaidia wakulima wauze mapema pamba yao mara baada ya kuivuna.
  • Kuhusu mizani, Waziri Mkuu aliiagiza wakala wa vipimo nchini (WMA) waende wakakague mizani ya kwenye AMCOS na kwenye vinu vya kuchambulia pamba (ginneries) kwa sbabu ya tofauti kubwa ya uzito inayojitokeza na kuwalazimisha wakulima kulipia upotevu wa kilo hizo.
  • Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe atume wakaguzi kwenye Bodi ya Pamba ili wabainishe matumizi ya sh.100 kwa kila kilo ambazo zimekuwa zikilipwa kwenye bodi hiyo.
Ad

Unaweza kuangalia pia

TUNATAKA MBEGU ZOTE ZIZALISHWE NCHINI – WAZIRI HASUNGA

Serikali imeeleza kuwa imekusudia kuanzisha juhudi wezeshi kuhakikisha kuwa mbegu bora za kilimo zinazalishwa nchini …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *