MAMENEJA WA TANESCO WATAKIWA KUTEMBELEA VIWANDA KWENYE MAENEO YAO

  • Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, ametoa Siku Saba kwa Mameneja wa TANESCO kote nchini kutembelea viwanda kwenye maeneo yao kwa lengo la kuhakikisha kuwa viwanda hivyo vinapata umeme wa uhakika kwa ajili ya uzalishaji na kufanya utatuzi endapo kutakuwa na changamoto ya kutokuwepo kwa umeme kwenye maeneo hayo.
  • Aliyasema hayo tarehe 18 Juni, 2019 wakati wa Mkutano wake na Jumuiya ya Wamiliki wa Viwanda ambapo kikao  hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Salum Shamte, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Mwanamani Kidaya, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka na watendaji wengine kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara na Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI).
TN
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Salum Shamte akizungumza wakati wa Mkutano wa Waziri wa Nishati na Jumuiya ya Wamiliki wa Viwanda uliofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga.
  • “Nimetoa Siku Saba za kutekeleza suala hili, na kama hawajatembelea maeneo yenu, wenye Viwanda toeni  taarifa ili tuweze kuchukua hatua lakini na ninyi wamiliki wa viwanda, hakikisheni kuwa mnalipa bili za umeme la sivyo tutakata umeme.” alisema Dkt Kalemani.
  • Kuhusu gharama za umeme aliagiza kuwa, TANESCO waendelee kutoa  gharama halisi za kumuunganishia mteja umeme na si kulimbikizia gharama hizo hali itakayochelewesha lengo la uanzishaji wa viwanda vingi nchini.
  • “Mkifanya makadirio ya gharama za umeme anazopaswa kulipia mteja hakikisheni kuwa mnaweka gharama halisi kwa sababu ikitokea umeagizwa kurudia kufanya makadirio hayohayo na yakashuka, Meneja, utachukuliwa hatua.” alisema Dkt Kalemani.
TN
Wadau mbalimbali waliohudhuria Mkutano wa Waziri wa Nishati na Jumuiya ya Wamiliki wa Viwanda uliofanyika jijini Dar es Salaam.
  • Kuhusu ushirikishaji wa Sekta binafsi kwenye Sekta ya Nishati, Dkt Kalemani alisema kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta hiyo kwani kukua kwa uchumi wa nchi kunategemea mashiriakiano kati ya pande hizo mbili.
  • kuhusu uanzishaji wa viwanda vijijini alitoa wito kwa wawekezaji hao kuainisha mapema maeneo watakayojenga viwanda wakati miradi ya umeme vijijini ikiendelea kutekelezwa ili kusogeza miundombinu ya umeme kwenye maeneo kabla ya viwanda kujengwa.
TN
Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga akizungumza jambo wakati wa Mkutano wa Waziri wa Nishati na Jumuiya ya Wamiliki wa Viwanda uliofanyika jijini Dar es Salaam.
  • kwa upande wake, Mwenyekiti wa TPSF, Salum Shamte, alimpongeza Waziri wa Nishati kwa kuitisha mkutano huo muhimu na kuweza kutoa maagizo ya papo kwa papo ya kutatua baadhi ya changamoto zilizoainishwa na wenye viwanda hao pia kwa kuahidi kutatua changamoto zote zilizoainishwa kwenye Mkutano huo.
TN 5-01
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa pili kushoto), Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua (wa kwanza kulia), Mwenyekiti wa TPSF, Salum Shamte (wa kwanza kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye (wa pili kutoka kulia) wakiwa katika Mkutano na wenye viwanda uliofanyika jijini Dar es Salaam.
  • Alitoa wito kwa Serikali kuzingatia suala la kuwapa kipaumbele wazawa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Nishati na kupongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuboresha hali ya umeme nchini kupitia miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme.
  • Kikao cha Waziri wa Nishati na wenye viwanda kililenga kusikiliza changamoto na maoni ya wenye viwanda hao kuhusu nishati ya umeme na Gesi na kujadiliana kuhusu utatuzi wake ambapo wadau hao walipata fursa ya kutoa maoni mbalimbali ambayo Wizara ya Nishati kupitia Taasisi zake iliahidi kuyafanyia kazi.
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *