SERIKALI YAJA NA MRADI MPYA WA UMEME

 • Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imezindua rasmi mradi mpya wa umeme unaolenga kupeleka nishati hiyo katika maeneo yaliyoko pembezoni mwa miji.
 • Waziri mwenye dhamana ya sekta hiyo, Dkt Medard Kalemani, kwa nyakati tofauti wiki hii, amezindua mradi husika unaojulikana kwa jina la kigeni kama ‘Peri-Urban’ katika Wilaya tofauti za Mkoa wa Pwani na kubainisha kuwa gharama ya wananchi kuunganishwa ni sawa na ile ya umeme vijijini yaani shilingi 27,000 tu.
 • Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Agosti 4, 2019, Dkt Kalemani alisema Serikali iliamua kuandaa mkakati maalum wa kupeleka umeme katika maeneo ya pembezoni mwa miji ambayo yalibainika kurukwa na miradi mbalimbali ya umeme.
EL 1-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza huku akiwa ameshika kibatari alichokabidhiwa na wananchi wa Mkuranga, mkoani Pwani wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa mradi mpya wa umeme ujulikanao kama ‘Peri-Urban’ Agosti 4, 2019. Kibatari hicho ni ishara ya wananchi wa Mkuranga kuachana na matumizi yake na kutumia umeme utakaounganishwa ndani ya kipindi cha miezi tisa.
 • “Mradi huu ni mahsusi kwa ajili ya maeneo ambayo yako mijini lakini yana sura ya vijiji; yaani yako pembezoni mwa miji.”
 • Alisema serikali imetumia gharama kubwa kutekeleza mradi huo hivyo akawataka wananchi katika maeneo yote ambako utatekelezwa, wachangamkie fursa hiyo kwa kujitokeza kwa wingi kulipia ili waunganishiwe umeme kisha wautumie kwa shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo.
 • Gharama za kutekeleza mradi huo wilayani Mkuranga ni shilingi bilioni 11.5, Wilaya ya Kisarawe shilingi bilioni 25 na Wilaya ya Kigamboni shilingi bilioni 9.32 ambazo zote ni fedha za ndani. Hizo ni Wilaya ambako tayari mradi umezinduliwa rasmi lakini zoezi hilo linaendelea katika maeneo mengine mbalimbali nchini.
EL 2-01
Wafanyakazi wa Kampuni ya Mkandarasi Namis Corporate Ltd, ambayo itatekeleza mradi mpya wa umeme ujulikanao kama ‘Peri-Urban’ wilayani Kisarawe, wakitambulishwa kwa wananchi wa Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa mradi huo wilayani humo, Agosti 3, 2019.
 • Katika Wilaya hizo tatu ambazo tayari Waziri amezindua mradi husika, alitoa maelekezo mahsusi kwa wakandarasi ambao wanatekeleza kazi hiyo. Miongoni mwa maagizo hayo ni kuhakikisha mradi unatekelezwa ndani ya kipindi kilichoainishwa katika mkataba ambacho ni miezi tisa.
 • “Hatutaongeza muda hata kidogo,” alisisitiza.
 • Vilevile, Waziri aliwataka wakandarasi husika, kuajiri wananchi wa maeneo husika ambako mradi unatekelezwa na kuwalipa ujira wao kwa wakati. Akifafanua, alisema ajira hizo ni zile zisizohitaji taaluma maalum kama vile kuchimba mashimo, kufukia nguzo na nyingine za aina hiyo.
EL 4-01
Sehemu ya umati wa wananchi wa Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani, wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa usambazaji umeme katika maeneo yaliyo pembezoni mwa miji, iliyofanyika wilayani humo Agosti 3, 2019.
 • Pia, aliagiza wananchi wenye nyumba zisizozidi vyumba vinne, wagawiwe vifaa vya Umeme Tayari (UMETA), ili kuwapunguzia gharama za kutandaza mfumo wa nyaya za umeme. Alisema vifaa hivyo vimetolewa bure na serikali kwa idadi ya 250 kila eneo na kwamba vikiisha, wananchi watauziwa kwa gharama ndogo ya shilingi 36,000 tu.
 • Viongozi mbalimbali wa maeneo ambako mradi umezinduliwa wakiwemo wa serikali na vyama vya siasa, wameipongeza serikali kwa kubuni  na kuanza kutekeleza mradi huo kutokana na uhitaji wa umeme waliokuwa nao wananchi wa maeneo husika.
 • Waziri alizindua mradi wa ‘Peri-Urban’ Agosti 4 (Mkuranga), Agosti 3 (Kisarawe) na Agosti 2 (Kigamboni), zote mwaka huu wa 2019. Mradi huo utazinduliwa wilayani Kibaha na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Agosti 5 ambapo zoezi litaendelea katika maeneo mengine mbalimbali.
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.