WANANCHI VIJIJINI RUKSA KULIPIA UMEME KWA KUDUNDULIZA

 • Wananchi wa maeneo ya vijijini ambao hawana uwezo wa kulipia shiingi 27,000 za kuunganishiwa umeme kwa mkupuo, sasa wanaweza kulipia huduma hiyo kwa kudunduliza kidogo kidogo.
 • Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani aliyasema hayo Disemba 3, 2019 kijijini Mnekezi, wilayani Chato, ambapo alikuwa akizungumza na wananchi kabla ya kuwasha rasmi umeme kijijini hapo.
3-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye miwani), akifuatana na Mkuu wa Wilaya ya Chato, Charles Kabeho (wa tatu-kulia), kwenda kuwasha umeme katika moja ya nyumba za wananchi wa kijiji cha Mnekezi, wilayani Chato, Mkoa wa Geita, Desemba 3, 2019.
 • Alikuwa akitoa maelekezo kwa wataalamu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwamba, wahakikishe wananchi wote wanaunganishiwa umeme bila kubagua hali zao kiuchumi kama ilivyo azma ya serikali.
 • Alisema kuwa, pamoja na serikali kupunguza gharama za kuunganisha umeme vijijini hadi shilingi elfu 27 tu lakini bado wako wananchi ambao kipato chao hakiwezi kuwaruhusu kulipa pesa hiyo kwa mkupuo, hivyo akawataka watendaji hao kupokea malipo ya wananchi husika kwa mtindo wa kudunduliza.
2-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati-mwenye kipaza sauti), akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mnekezi, wilayani Chato, Mkoa wa Geita, kabla ya kuwasha rasmi umeme kijijini hapo, Desemba 3, 2019. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Chato, Charles Kabeho.
 • “Akipata elfu 10 akaleta, pokea umwandike; kesho akileta nyingine elfu tano pokea hadi pale atakapotimiza kiwango kinachotakiwa cha elfu 27.”
 • Katika hatua nyingine, Waziri alitoa hamasa kwa wananchi wa kijiji hicho na vingine vyote nchini ambako miradi mbalimbali ya umeme inatekelezwa, kutochagua kazi.
 • Alitoa hamasa hiyo baada ya kutoa maagizo kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchi nzima, kuhakikisha wanaajiri vibarua kutoka maeneo husika ili kuharakisha kazi lakini pia kuinua kipato cha wananchi, hususan vijana wa maeneo hayo.
4-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akitoa maelekezo kwa wafanyakazi wa mkandarasi wa umeme vijijini, anayetekeleza mradi huo katika kijiji cha Mnekezi, wilayani Chato, Mkoa wa Geita, akiwa katika ziara ya kazi, Desemba 3, 2019. Waziri aliwasha rasmi umeme katika kijiji hicho.
 • Aidha, aliwataka wananchi kuachana na kasumba ya kulalamika kuwa hawajaunganishiwa umeme wakati hawajalipia huduma husika kwa visingizio tofauti, ikiwemo madai ya ukosefu wa nguzo.
 • “Wananchi, suala hili narudia tena kulisemea; ninyi mnachotakiwa kufanya ili muunganishiwe umeme ni kulipia tu na kuandaa nyumba zenu kwa kuweka mfumo wa nyaya. Suala la nguzo na vifaa vingine haliwahusu. Lipieni ili mletewe umeme,” alisisitiza.
5-01
Wafanyakazi wa kampuni ya mkandarasi wa umeme vijijini ambaye anatekeleza mradi huo katika kijiji cha Mnekezi, wilayani Chato, wakiendelea na kazi husika, baada ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), kukagua kazi hiyo na baadaye kuwasha rasmi umeme katika kijiji hicho.
 • Waziri Kalemani, ambaye pia ni Mbunge wa eneo husika (Chato), aligawa kwa wananchi wa Mnekezi, vifaa 50 vya Umeme Tayari (UMETA) bure, mbali na vile 250 ambavyo kila mkandarasi wa miradi ya umeme vijijini hutakiwa kugawa katika eneo lake.
 • Katika ziara hiyo, Waziri alifuatana na viongozi mbalimbali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Chato, Charles Kabeho.
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *