NAIBU WAZIRI MGALU ALIRIDHISHWA NA MIUNDOMBINU YA UMEME MRADI SGR

  • Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema ameridhishwa na ujenzi wa miundombinu ya njia ya kusafirisha umeme wa kV 220 inayoendelea kujengwa katika Reli ya kisasa kutoka jijini Dar es salaam hadi mkoani Morogoro.
1-01
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( mwenye kilemba) akiangalia kazi ujenzi wa msingi wa kusimika nguzo kubwa ya umeme wa kV 220 utakaotumika katika reli ya kisasa, unayoendelea katika njia ya kusafirisha umeme.
  • Mgalu alieleza hayo Desemba 7,2019 baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ujenzi wa miundombinu hiyo kuanzia Kituo cha Kinyerenzi, Pugu hadi Kisarawe  jijini Dar es salaam ambapo asilimia 70 ya kazi hiyo imekamilika.
  • Alitumia ziara hiyo kuwathibitishia watanzania kuwa mradi huo wa ujenzi wa njia ya umeme utakamilika kwa wakati kulinga na makubaliano ya mkataba na umeme upo mwingi na wa kutosha kuwezesha reli hiyo kufanya kazi yake wakati wote.
2-01
Mafundi wakiendela na kazi ya kumwaga zege chini ardhini ikiwa ni ujenzi wa msingi wa nguzo ya kusafirisha umeme mkubwa utakaotumika katika reli ya kisasa.
  • Alifafanua kuwa ujenzi wa miundombinu ya njia ya kusafirisha umeme inatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2020 ili kutoa fursa ya kuanza majaribio ya safari kwa kutumia Treni ya umeme, kabla ya kuanza rasmi kwa safari hizo mwezi Julai, 2020.
  • “Niwatoe hofu wale wote wenye mashaka na usafiri wa reli kwa kutumia umeme, umeme upo mwingi na wa kutosha nchini, kwa sasa tunazalisha zaidi ya megawati 1601, tunazotumia ni megawati 1116 tu, pia kazi ya kujenga miradi mikubwa ya kuzalisha umeme mwingi zaidi inaendelea,  ukiwemo Mradi wa Julias Nyerere katika bonde la mto Rufiji, Rusumo na Kinyerezi”, alisisitiza Mgalu.
3-01
Mafundi wakendelea wakiendelea na kazi ya kusuka nondo kabla ya kumwaga zege, katika ujenzi wa msingi wa nguzo ya kubwa ya kusafirisha umeme wa kV 220, utakaotumika katika reli ya kisasa.
  • Pia alikagua ghala za kuhifadhia vifaa mbalimbali vinavyotumika katika ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme lililopo Kibaha mkoani Pwani na kushuhudia uwepo wa vifaa vya kutosha kukamilisha ujenzi wa njia hiyo.
  • Aidha aliwataka wasimamizi wa mradi huo kuwalipa vizuri wafanyakazi /vibarua wanaofanya kazi katika mradi huo ili na wao wafurahie na kunufaika kuwepo kwa mradi huo, vilevile aliwataka vibarua hao kufanya kazi kwa bidii, kuwa walinzi wa vifaa hivyo na miundombinu na kuweka mbele maslahi ya taifa.
4-01
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akitoa maelekezo kwa wasimamizi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa utakaotumika katika reli ya kisasa baada ya kutembelea na kukagua ghala la kuhifadhia vifaa hivyo lililopo Kibaha, mkoani Pwani.
  • Aidha alilipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya njia ya kusafirisha umeme mkubwa  katika reli ya kisasa, na kuwataka kuongeza kasi zaidi ya ujenzi huo ili ikiwezekana ujenzi huo ukamilike kabla ya muda waliopewa.
5-01
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza na baadhi ya wafanyakazi/ vibarua katika ghala la kuhifadhi vifaa vya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa utakaotumika katika reli ya kisasa, lililopo Kibaha, mkaoani Pwani.
  • Kwa upande msimamizi wa mradi huo kutoka Tanesco, Mhandisi Deogratius Msaki alisema kuwa kazi hiyo inaendelea vizuri licha ya changamoto ya kigiografia ya ardhi katika baadhi ya maeneo na hali ya hewa ya mvua.
  • Aliweka wazi kuwa mpaka sasa tayari wamesimamisha  nguzo zaidi 120 kati ya 456 zitakazotumika kutoka  Dar es salaam hadi Morogoro, pia kazi ya kuweka vikombe na kuanza kuvuta nyaya imekwisha anza katika maeneo ambayo tayari usimikwaji wa nguzo umekamilika huku kazi hiyo ikiendelea, matarajio yao ni kuukabidhi mradi huo Tar 28 Februari 2020.
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.