- Serikali imepongezwa kwa kuwezesha wananchi kufikiwa na huduma ya majisafi na salama baada ya miaka zaidi ya hamsini bila kuwepo kwa huduma hiyo katika eneo lao.
- Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso mwishoni mwa wiki wakati akizindua mradi wa maji katika jijiji cha Makang’a, jimbo la Mtera mkoani Dodoma utakaonufaisha wananchi zaidi ya elfu saba na mia tano.
- “Mradi huu umetumia milioni 350 tu wakati tungetumia mkandarasi ingetumia zaidi milioni 600 na utaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi katika eneo lenu na hii ndiyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kuwa wananchi wote mnapata maji safi na salama,” alisisistza Aweso.
- Akifafanua, Naibu Waziri Aweso amesema kuwa mradi huo umetekelezwa na wataalamu wa ndani kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DUWASA) ikiwa ndio dhamira ya Serikali kupitia Wizara ya maji kutekeleza miradi ya maji hasa vijijini kwa kutumia wataalamu wa ndani.
- “Serikali ya Awamu ya Tano inawajali wananchi wake hivyo pamoja na kukamilika kwa mradi huu tumeshatoa fedha nyingine kiasi cha shilingi milioni miamoja ziko kwenye akaunti tayari kwa ajili ya kuchimba visima viwili, hivyo wataalamu wetu watakuja hapa jumatatu tarehe 11 kufanya utafiti wa maeneo vitakapochimbwa visima hivyo”, alisisitiza Aweso.
- Wananchi wote hakikisheni mnautunza mradi huu ili unufaishe hata vizazi vijavyo kwa kuwa fedha nyingi zimetumika katika kuutekeleza.
- Naye, Mkurugenzi wa DUWASA Mhandisi David Palangyo amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa tarehe 19 Septemba2019 na umehusisha ujenzi wa vituo kumi na tatu (13) vya kuchotea maji kwenye maeneo mbalimbali katika Kijiji hicho, kununua na kufunga pampu zenye uwezo wa kuzalisha lita laki tatu na thelathini na sita kwa siku, mfumo wa nguvu za jua kwa ajili ya kuendesha pampu hizo, ununuzi na ulazaji wa mabomba ya plastiki na viungio vyake.
- Kazi nyingine ni uchimbaji na ufukiaji wa mabomba ya plastiki ya class C na viungio vyake na kulaza mabomba yenye vipenyo vya ichi 1.5 hadi inchi 6 kwa jumla ya urefu wa meta zaidi ya elfu kumi na tatu.
- Akizungumzia mafaniko ya mradi huo, Mhandisi Palangyo amesema kuwa wananchi wote wa Kijii cha Makangw’a sasa wanapata maji ya bomba na pia wananchi walishirikishwa katika mradi huo kuanzia kuchagua maeneo ya kujenga vituo vya kuchotea maji na hata utekelezaji wa mradi huo.
- Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo hilo Livingstone Lusinde amesema kuwa wananchi wanaonufaika na mradi huo wanaowajibu wa kutunza mradi huo ili usihujumiwe.
- Kwa upande wa viongozi watakaosimamia mradi huo wametakiwa kuhakikisha wanasoma mapato na matumizi ya mradi huo na kutunza fedha zitakazotokana na mradi huo benki ili uwe endelevu.
- Kabla ya kutekelezwa kwa mradi huo hali ya upatikanaji wa maji katika Kijiji cha Makangw’a ilikuwa siyo wa kuridhisha, maji ya bomba yalikuwa yanapatikana katika kitongoji kimoja tu kati ya 11 na yaliwekwa na mwekezaji binafsi mwaka 2016.
Ad