KITUO CHA AFYA BWISYA CHAPANDISHWA HADHI KUWA HOSPITALI YA WILAYA – MAJALIWA

Rais Dkt. John Pombe Magufuli amepandisha hadhi ya kituo cha afya cha Bwisya kilichoko Ukara wilayani Ukerewe, Mwanza kiwe na hadhi ya hospitali ya wilaya kuanzia leo.

Hayo yamesemwa na mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Bwisya kwenye mkutano uliofanyika viwanja vya bandarini Jumatano, Septemba 23, 2020.

Ad

Amesema awali kituo hicho cha afya zamani kilikuwa zahanati lakini ikapandishwa hadhi ili kuwasaidia wakazi wa tarafa ya Ukara. “Tunataka wananchi wasihangaike kwenda hadi Nansio yalipo makao makuu ya wilaya hii. Huduma zitatolewa hapahapa. Hiyo maana yake, majengo ya tiba yataongezwa na vitengo vya huduma vitaongezwa, na madaktari bingwa wataletwa wakae hapa.”

Amesema ili kufanikisha hilo kwa haraka hospitali ya wilaya ya Ukerewe ambayo iko Nansio nayo pia itapandishwa na kuwa na hadhi ya hospitali ya mkoa. Kupandishwa hadhi kwa kituo hicho cha afya, kutawasadia wakazi wa Ukara ambao walikuwa wanapaswa kufuata huduma za rufaa Nansio ambako ni umbali km 30 au Mwanza mjini ambako ni umbali wa km. 75.9.

“Hapa Bwisya zililetwa sh. bilioni 1.4 za kupandisha hadhi kutoka zahanati na kufikia kuwa kituo cha afya. Hospitali nyingi za wilaya hapa nchini zimepatiwa sh. bilioni 1.8, kwa hiyo na ninyi hapa mtapatiwa fedha ili majengo yanayohitajika yaweze kukamilika,” amesema.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mwanza kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kumwombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi na diwani wa kata ya Bwisya, Bw. Dickson Sute. Madiwani wengine watatu wa tarafa ya Ukara, wamepita bila kupingwa.

Akitoa ufafanuzi kwenye sekta hiyo ya afya, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh. bilioni 2.95 zimetolewa wilaya ya Ukerewe kwa ajili ya ujenzi wa majengo tano ambayo ni maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya wazazi, chumba cha kuhifadhia maiti na nyumba ya mganga  katika vituo vya afya vya Bwisya, Kagunguli na Muriti.

“Kituo cha Afya cha Bwisya kilipatiwa shilingi bilioni 1.4 ambapo ujenzi na upanuzi umekamilika. Kituo cha Afya Kagunguli kilipatiwa shilingi milioni 322 ambapo ujenzi chumba cha kisasa cha upasuaji umekamilika na Kituo cha Afya Muriti kilipatiwa shilingi milioni 967 ambapo ujenzi majengo ya RCH, upasuaji na wodi ya wazazi yote yamekamilika,” amesema.

Kuhusu ununuzi wa dawa na vifaa tiba, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh. bilioni 3.9zimetolewa kwa ununuzi wa dawa na vifaa tiba kwa kipindi cha 2015/2016 – 2019/2020 ambapo wastani wa bajeti ya dawa kwa mwezi ulikuwa ni shilingi milioni 63.

Kuhusu kuimarisha usafiri wa majini katika maziwa mito na bahari kama ilivyoainishwa kwenue Ilani ya Uchaguzi uk. 69 -70, Mheshimiwa Majaliwa amesema ujenzi wa vivuko vinne ambavyo vitatoa huduma katika maeneo ya Bugolora – Ukara (Mwanza), Kayenze – Bezi (Mwanza), Nyamisati – Mafia (Pwani) na Nkome – Chato -Buharamba (Geita) unaoendelea.

Amesema Serikali imekamilisha ununuzi wa boti tatu za uokozi kwa ajili ya maeneo ya Ilugwa – Ukara (Ukerewe), Nafuba na Gana katika kisiwa cha Ukerewe. “Ili kuimarisha usafiri katika maziwa na mito, Serikali imeanza ujenzi wa vivuko na maegesho muhimu nchini ikiwemo Ujenzi wa maegesho ya Ilugwa (Ukerewe) pamoja na vivuko vya Bwiro–Bukondo (Ukerewe), Irugwa–Murutanga (Ukererwe) na Kakuro–Gana (Ukerewe). Na hii iko kwenye ukurasa wa 83 wa Ilani yetu,” amesema.

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *