DKT. KALEMANI APIGA MARUFUKU MKANDARASI KUPEWA KAZI ZA REA ZAIDI YA MKOA MMOJA

Na Zuena Msuya na Hafsa Omari, Tabora

Waziri wa  Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema kuanzia sasa  ni marufuku kwa wakandarasi watakaotekeleza miradi Ya usambazaji wa umeme vijijini( REA), kupewa kazi katika mikoa miwili na badala yake sasa watapewa kwa kila wilaya bila kujali idadi ya vijiji vilivyopo.

Ad

Dkt. Kalemani alisema hayo nyakati tofauti, mkoani Tabora alipokuwa akizindua rasmi mradi wa usambazaji wa umeme katika kila Kitongoji nchini uliofanyika katika wilaya za Uyui na Nzega mkoani humo, Septemba 24, 2020 ambapo alisema kuwa mradi huo utavifikia vitongoji vyote nchini bila kujali kuwa kimefikiwa na umeme au laa.

Alisema kuwa lengo la kuwapatia wakandarasi hao kazi za wilaya ni kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa haraka ndani ya muda mfupi na kwa wakati.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Ufuruma, Kijiji cha Ufuruma,Wilaya ya Uyui,Mkoani Tabora,wakati akiwa kwenye uzinduzi wa mradi wa Usambazaji umeme kwa kila kitongoji nchini, uliofanyika Septemba 24,2020.

“Kuanzia sasa Wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya REA nchini, watakuwa wanapewa kazi za kutekeleza miradi hiyo kwa kila wilaya bila kujali idadi ya vijiji vilivyopo,kwa maana kwamba  mkandarasi anaweza pewa wilaya moja yenye  vijiji ishirini au sabini,jukumu lake ni kumaliza kwa wakati, hii itaondoa changamoto ya kutomaliza miradi kwa wakati, au wengine walikuwa wanaelekeza nguvu nyingi katika eneo A, na kuacha eneo B, ama kufanya maeneo yote kwa kusuasua”, alisema Dkt. Kalemani.

Alieleza kuwa utaratibu huo utawezesha ukamilishaji wa miradi ya namna hiyo kwa wakati na kwamba mkandarasi yeyote atakayechelewesha mradi atachukuliwa hatua za kimkataba, kisheria na za kiusimamizi kwakuwa maeneo ya utekelezaji wa miradi imepunguzwa tofauti na awali.

Vilevile alisema kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza kwa yeyote atayechelewesha mradi na badala yake atakatwa asilimia 10% ya fedha zake kama adhabu na mradi huo atapewa mtu mwingine.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani(mwenye shati la bluu) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye uzinduzi wa Usambazaji wa umeme kwa kila kitongoji nchini uliofanyika katika Kitongoji cha Ufuruma, Kijiji cha Ufuruma,Wilaya ya Uyui,Mkoani Tabora, Septemba 24,2020,(kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt.Philemon Sengati(kulia) Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati vijiji(REA) Wakili Julius Kalolo.

“Hatua hii itaondoa visingizio na sababu za baadhi ya wakandarasi wenye tabia hiyo kwa lengo la kuchelewesha mradi, kwa sababu wengine walikuwa wanasingizia ukubwa wa eneo, wengine miundombinu au vifaa havitoshi ana kufika kwa wakati, sasa hii itamaliza sababu zote za kuchelewesha miradi”, alisisitiza Dkt. Kalemani.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani alilisisitiza Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO) kuwakatia umeme wateja wenye madeni sugu ili ikupata fedha za kulijengea uwezo shirika hilo kutoa huduma bora na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

“Endapo kuna Taasisi au Shirika la Umma linadaiwa ndani ya siku 14 msiwaoneee aibu, nendeni makakate umeme, na wakiwapigia simu kuomba kurudishiwa msikubali, na mimi nikipigiwa sitaruhusu waunganishwe hadi pale watakapokuwa wamelipia”, alisema Dkt. Kalemani.

Aliwagiza Mameneja wa Kanda, Mikoa Wilaya kutowaonea huruma wateja wa namana hiyo kwa kuwa wanarudisha nyuma maendeleo ya shirika hilo na kusababisha wananchi wengine kukosa huduma bora kwa wakati.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Je! Wajua Mchango wa Madini ya Tanzanite katika Pato la Taifa?

Madini ya Tanzanite, yanayopatikana pekee katika eneo dogo la Mererani, Tanzania, ni miongoni mwa rasilimali …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *